Hadija omary, Lindi
Wakulima wa ufuta na wanachama wa Chama kikuu cha Ushirika (Runali) kinachojumuisha wakulima wa Ruangwa, Nachingwea na Liwale mkoani Lindi, wamekumbushwa kuendelea kuweka ufuta wao katika hali ya usafi ili kuendelea kupata bei mzuri.
Rai hiyo imetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Sara Chiwamba katika kijiji cha Nangano alipokuwa anazungumza na wakulima waliokwenda kushuhudia mnada wa tano wa ufuta wa chama hicho.
Katika mnada huo Jumla ya tani 3050 na kilo 132 zilifikishwa mnadani ambapo makampuni 13 yalijitokeza kununua huku makampuni saba pekee ndio yaliyoshinda kununua mzigo huo kwa bei ya juu ya Sh. 1,867 na bei ya chini Sh. 1,863.
Chiwamba alisema bei wanazozipata sasa zinatokana pia ubora na usafi wa ufuta wao hivyo ni vyema kuendelea kuweka katika hali hiyo ili kuendelea kupata bei mzuri kutoka kwa wanunuzi.
Pamoja na msisitizo huo Chiwamba aliwapongeza wakulima kwa kupeleka ufuta wao katika hali ya usafi tofauti na hapo awali wakati msimu wa mauzo unaanza ambapo hali ya usafi wa ufuta wao ilikuwa sio ya kuridhisha.
“Wakati ninakuja huku nimepita katika maghala tofauti tofauti na nikaja kumalizia hapa kwa kweli ufuta ni msafi hongereni sana, ninaomba nitoe shime tuendelee kuleta ufuta msafi isije ikafika dakika ya mwisho ukasema sasa ngoja nimalizie vyote na mavumbi yote ya shambani na kila kitu haitakuwa na maana,” alieleza chiwamba.