JERUSALEM, ISRAEL
ISRAEL jana imezindua satelaiti mpya ya ujasusi, inayosemwa itaiwezesha idara yake ya jeshi kuhusu intelijensia kupata taarifa bora za ujasusi.
Nchi hiyo imekuwa ikiimarisha uwezo wake wa kijasusi ili kuwachunguza maadui zake kama vile Iran ambayo inautizama mpango wake wa nyuklia kama kitisho.
Satelaiti hiyo kwa jina Ofek 16, ilirushwa kuelekea anga za juu mapema jana, kutoka eneo la kati la Israel kwa kutumia kombora lililotengenezwa ndani ya Israel, ambalo limekuwa likitumika kurusha satelaiti za awali nchini humo.
Wizara ya Ulinzi ya Israel imeitaja Ofek 16 kuwa na uwezo ulioimarishwa zaidi wa uchunguzi wa kijeshi.
Picha za kwanza za Satelaiti hiyo zinatarajiwa baada ya takriban wiki moja.