WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM
SERIKALI imeizuia JKT Tanzania kucheza mechi zake zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara mbele ya mashabiki kutokana na kukiuka mwongozo wa afya michezoni ilipovaana na Yanga.
JKT Tanzania inayotumia Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, juzi ilicheza na Yanga na kuambulia sare ya bao 1-1, mchezo ulioshudiwa na idadi kubwa ya mashabiki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Lorietha Lawrence, katika mchezo huo namba 288, mashabiki walijazana uwanjani na kukaa bila kuzingatia kanuni ya 2.0.2 inayosisitiza kuachiana mita moja.
Katika taarifa hiyo, Lorietha, alieleza kuwa uchunguzi umebaini kuwa wawakilishi wa timu mwenyeji, waliokuwa wanadhibiti mageti, hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Alisema kuwa wasimamizi hao wa getini, waliruhusu mashabiki wenye tiketi na wasikuwa nazo kuingia uwanjani na kuharibu mpangilio wa ukaaji ambao ulikuwa umezingatiwa vizuri hadi saa nane mchana.
“Hatua hii inalenga kuzikumbusha klabu mwenyeji, wasimamizi wa michezo na wadau wengine kote nchini kuendelea kusimamia kikamilifu mwongozo wa afya na taratibu nyingine michezo hadi pale Serikali itakapojiridhisha kuwa ugonjwa wa Covid-19 umekwisha,” ilisema taarifa hiyo.
Alisema lengo ni kuwalinda wachezaji, viongozi na wananchi wote, hivyo Serikali itaendelea kuchukua hatua kali zaidi kwa wale watakaondelea kukaidi.