Gurian Adolf -Sumbawanga
MAHAKAMA ya Wilaya ya Sumbawanga imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mkazi wa Kitongoji cha Kizwite, Samson Venance (27), baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kubaka msichana mwenye umri wa miaka 18.
Pia mtuhumiwa ametakiwa kulipa faini ya Sh milioni 3 kwa kutenda kosa hilo kinyume na sheria.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Jacob Ndira alitoa hukumu hiyo jana, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Simon Peres.
Katika shauri hilo, mwendesha mashtaka aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo, Januari 17, mwaka huu saa 8 usiku huko Kizwite ambako ndiko yaliko makazi yake.
Peres alidai kuwa mbakaji alienda nyumbani kwa binti huyo ambaye wazazi wake hawakuwepo nyumbani na kumgongea mlango, alipofungua alimkamata kwa nguvu na kuanza kumbaka.
Alidai mwathirika alipiga kelele za kuomba msaada, ndipo baadhi ya majirani walijitokeza na kumsaidia kumkamata mtuhumiwa na kumpeleka polisi.
Awali Venance aliposomewa mashtaka yake alikana kuhusika na tukio hilo, lakini alitiwa hatiani baada ya upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake, ikiwemo kutoa vipimo vya hospitali vilivyoonyesha kitendo hicho kilifanyika.
Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiambia mahakama usiku ule alikuwa amelewa pombe na hivyo hakumbuki alichokifanya.
Wakili wa Serikali, Peres aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo vya ubakaji kitu ambacho ni kinyume na sheria.
Hakimu Ndira alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo kuacha shaka, mahakama hiyo imemkuta na hatia Venance hivyo kwa kutumia kifungu 130, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (E), pia kifungu 131, (I) Sura ya 16, kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2020, inamhukumu kwenda jela miaka 30 na kulipa faini ya Sh milioni 3.