32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Mwanza waaswa kuchangamkia kampeni ya elimu kwa mlipakodi

Veronica Kazimoto, Mwanza 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani hapa kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku wafanyabiashara hao wakiishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa zoezi hilo ambalo linawaleta karibu walipakodi na wakusanya kodi.  
 
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni hiyo ambayo imeanza June 15 hadi 22 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa, ni muhimu wafanyabiashara wote wakalipa kipaumbele suala la ulipaji kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii kwa manufaa ya kila Mtanzania.
 
“Kama mnavyojua umuhimu wa kodi na hasa katika kipindi hiki cha awamu ya tano hakuna Mtanzania ambaye hajashuhudia umuhimu wa kodi, tumeona barabara zikijengwa, ndege zikinunuliwa, ujenzi wa vituo vya afya, meli zikijengwa, ukarabati wa viwanja vya ndege ambavyo vyote vimesababishwa na uwezo wa serikali ambao umejengeka kwa mapato ya ndani,” alisema Mongella.
 
Mongella amesema kwamba, kutokana na faida hizo za kodi, ni muhimu wafanyabiashara wote wakatoa ushirikiano kwa maafisa hao wa TRA watakaopita katika maeneo ya biashara zao wakifanya zoezi hili la kutoa elimu ya kodi na kutumia fursa hiyo kupata uelewa na hatimaye waweze kulipa kodi ipasavyo na kwa wakati.
 
Amesema zoezi hilo limelenga kuwafikia wananchi na wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali mkoani hapa yakiwemo Rwagasore, Pamba road, Buhongwa, Nyerere road, Misungwi, Mwaloni na Kisesa.
 
Sambamba na hayo amesema mambo yote yamefanikiwa kutokana na uadilifu na utendaji kazi wenye tija uliofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kusimamia mapato ya ndani na kuyaelekeza katika kuimarisha uchumi wa nchi.
 
Naye Charles Lyamuya mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi maeneo ya mtaa wa Lumumba jijini Mwanza ameomba zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi liwe endelevu kutokana na kuwa linajenga urafiki baina yao na TRA na kwamba litaongeza uhiari wa kulipa kodi kwa wakati.
 
“Kutokana na elimu hii hakika tutalipa kodi ipasavyo kwa sababu inatuweka karibu na TRA suala ambalo linatuondolea hofu na pia tunaomba elimu hii iwe endelevu ili wafanyabiashara wengi waweze kujijenga zaidi na kuimarika katika biashara zao,” alisema Lyamuya.
 
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani Mwanza inafanyika pia katika Mkoa wa Morogoro na Mbeya na imelenga kuwaelimisha walipakodi juu ya mambo mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja na kupokea maoni, kusikiliza kero na changamoto za walipakodi hao ili kuzitafutia ufumbuzi.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles