33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Mbeya watakiwa kutumia fursa ya elimu kwa mlipakodi

Mwandishi wetu, Mbeya

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara na watoa huduma zinazolipiwa kodi mkoani Mbeya kutumia fursa ya kuongeza uelewa wa masuala ya ulipaji kodi kutoka kwa maofisa wa TRA wanaowatembelea madukani na katika maeneo yao ya kutolea huduma kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi.

Akizungumza wakati wa kuanza kampeni maalumu ya kuhamasisha ulipaji kodi mkoa wa Mbeya, Kaimu Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Stephen Kauzeni amesema lengo la kuwatembelea wafanyabiashara katika maeneo yao ni kuwapa elimu ya kodi bila kuathiri shughuli zao za uzalishaji kwa kuwa hawalazimiki kufunga na kwenda katika ofisi za TRA.

“Ni ombi letu kwa wafanyabiashara na watoa huduma watumie vilivyo fursa hii ya kupelekewa elimu ya kodi katika maeneo yao, hivyo basi, waulize maswali yote yanayohusu kodi zinazosimamiwa na TRA ili waweze kuongeza uelewa wa masuala ya ulipaji kodi”, amesema Kauzeni.

Amesema huduma zinazolipiwa kodi ni huduma zote zinazotolewa wa wataalamu wa fani mbalimbali ambapo sheria ya Usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 inawataka kujisajili, kuwa na namba ya utambulisho wa mlipakodi na kutumia mashine ya kieletroniki ya kutolea risiti (EFD) kwa wateja wao.

Amesema kuwa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodi katika mkoa wa Mbeya itafanyika kwa muda wa wiki moja kuanzia Juni 15 hadi 21 ambapo maofisa wa TRA watawatembelea wafanyabiashara katika maeneo yao ya biashara hususani maeneo yenye biashara nyingi ili kuwapatia elimu ya kodi na kuwaelekeza namna rahisi ya kulipa kodi kwa njia za mtandao wa kielektroniki.

Kauzeni ameongeza kuwa kitendo cha maofisa kutoa elimu katika sehemu za biashara pia inasaidia maofisa kuona biashara zinazofanyika na vile vile kumwelekeza mlipakodi namna nzuri ya kupanga ulipaji wa kodi zake kwa wakati bila kuathiri mwenendo wa biashara na kuepuka adhabu za kuchelewa kulipa kodi stahiki.

Amesema mbali na manispaa ya Mbeya mjini, maofisa wa TRA watawatembelea wafanyabishara katika wilaya za Rugwe, Kyela, Mbalali na Chunya pamoja na halmashauri ya Mbeya vijijini.

Naye Gwakisa Kibona ambaye ni wakili wa kujitegemea katika mji mdogo wa Mbalizi halmashauri ya Mbeya Vijijini amesema kuwa zoezi hilo linalofanywa na TRA ni zuri na kwamba kuanzisha aina hiyo ya utoaji elimu ya kodi kwa kuwatembelea katika maeneo yao ya biashara inaokoa muda na kuongeza uelewa wa ulipaji kodi miongoni mwa wafanyabishara.

“Kwa kweli nimefurahishwa na hatua hii ya ofisi ya serikali kwa maana ya TRA, kututembelea kwa ajili ya kutupa elimu ya kodi na nawashauri watoa huduma wenzangu na wafanyabishara kwa ujumla tutumie fursa hii vizuri tuongeze uelewa wa masuala ya kodi na mwisho wa siku tulipe kodi kwa wakati”, amesema Gwakisa Kibona wakili wa kujitegemea kutoka Mbalizi.

TRA imeanzisha kampeni maalumu ya kuhamasisha ulipaji kodi kabla ya tarehe 30 juini, 2020 nchi nzima kutokana na kuwa tarehe hiyo ndiyo mwisho wa mwaka wa fedha wa serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles