25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Zaidi ya wafanyabiashara 2000 wapatiwa elimu ya kodi Ilala

Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

ZAIDI ya wafanyabiashara 2000 katika mkoa wa kodi wa Ilala wamepatiwa elimu ya kodi inayoendelea katika mikoa mbalimbali nchini.
Mamlaka hiyo imekuwa na ikifanya kampeni ya elimu ya kodi mara kwa mara kwa kuwafata wafanyabiashara kwenye biashara zao (mlango kwa mlango).

Akizungumzai zoezi hilo Afisa Msimamizi wa Kodi wa mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zakeo Kowelo alisema kuwa katika siku sita za zoezi hilo, jumla ya wafanyabiashara 2,165 wamepatiwa elimu mbalimbali ya kodi.

Alisema maeneo ambayo wamewafikia wafanyabiashara na kuwapatia elimu ni Tabata, Relini, Bima, Liwiti, Barakuda, Kimanga, Segerea, Kinyerezi, Kisiwani na Bonyokwa Mkoa wa Kodi wa Ilala.

Alisema zoezi limeenda vizuri na kwamba wafanyabiashara wametoa ushirikiano wa kutosha kwa kutoa taarifa muhimu na kuonyesha nyaraka ambazo zilihitajika jambo ambalo limewawezesha kuwapa ushauri na elimu inayostahili.

“Kwa hili tunawashukuru sana kwani tumeweza kuwaelimisha kama tulivyopanga”, alisema Kowelo
Alisema zoezi lilihusisha kupita duka kwa duka na kuangalia taarifa za wafanyabiashara za kodi ambapo baada ya kuangalia taarifa walifanya majadiliano na kumshauri mfanyabiashara jinsi ya kutunza kumbukumbu.

Aliongeza kuwa kwa wale ambao hawajasajili biashara zao wameelekezwa taratibu za kusajili ili watambulike kuwa walipakodi na kwamba pamoja na kusajili biashara pia wafanyabiashara wameshauriwa jinsi ya kujisajili na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na wale wanaostahili kutumia mashine za kodi za kielektroniki wamepewa utaratibu wa kupata na kuzitumia mashine hizo.

“TRA ni sehemu ya biashara za wananchi hivyo lengo letu ni kuwaelimisha wananchi ili wafanye biashara kwa usalama zaidi na kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi sahihi na kwa wakati’, alisema Kowelo.

Naye Stewart Kimbaga mfanyabiashara wa duka la urembo maeneo ya Bonyokwa alisema kuwa kampeni hiyo ya elimu ya kodi ni nzuri na kwamba itasaidia kutokana na kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawana uelewa wa jinsi ya kufanya biashara ikiwa ni pamoja na utaratibu mzima wa kulipa kodi.

Alisema hiyo ni fursa muhimu na kwamba ukaguzi peke yake hautoshi bali unatakiwa uambatane na elimu ili kuwaongezea wananchi uelewa na kujenga uhusiano mzuri baina ya TRA na walipakodi.

Zoezi la kutembelea walipakodi katika maeneo yao ya biashara ni mkakati ambao TRA inautekeleza ili kuwaelimisha walipakodi, kuwapa ushauri wa kitaalamu kuhusu taratibu za kulipa kodi, kusajili biashara ambazo hazijasajiliwa, kuwakumbusha kulipa kodi, kutatua changamoto zinazo wakabili na kupata maoni yao kuhusu huduma inayotolewa na TRA kwa ajili ya kuboresha utendaji wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles