25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mataifa ya Afrika yaomba mjadala kuhusu ubaguzi

GENIVA, USWISI 

MATAIAFA 54 ya Afrika yamesaini barua ya kuliomba baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa kuitisha mjadala wa dharura kuhusu ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi.

Balozi wa Burkina Faso kwenye Umoja wa Mataifa, mjini Geneva ameandika barua hiyo kwa niaba ya mataifa hayo 54 ya Afrika, kuomba chombo hicho cha juu cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia masuala ya haki za binadamu kuanzisha mjadala huo wa dharura kuhusiana na ukiukwaji wa haki za binaadamu unaotokana na ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika na vitendo vya ukatili dhidi ya waandamanaji wanaoshinikiza kuondolewa kwa vitendo hivyo vya ukatili.

Barua hiyo inaomba mjadala huo kufanyika wiki ijayo wakati baraza hilo litakaporejea kwenye kikao chake cha 43, baada ya kusimamishwa kutokana na janga la virusi vya corona.

Ombi  hilo limetolewa baada ya ya familia ya Floyd jamaa wa wahanga wa ukatili wa polisi pamoja na takriban mashirika yasiyo ya kiserikali 600 kuliomba baraza hilo kuzungumzia kwa dharura suala hilo la ubaguzi wa kimfumo na ukatili wa polisi.

Ili ombi kama hilo liweze kukubaliwa na baraza hilo, linahitaji kuungwa mkono na angalau taifa moja.

Na kwa kuwa wito kama huo unatolewa na idadi kubwa ya mataifa, ni dhahiri kwamba inaongeza fursa ya kufanyika kwa mjadala huo, msemaji wa baraza hilo ameliambia shirika la habari la nchini Ufaransa, AFP.

George Floyd, 46, mmarekani mweusi ambaye hakuwa na silaha aliuawa akiwa mikononi mwa polisi, mjini Minneapolis nchini Marekani, Mei 25 baada ya ofisa wa polisi, Dereck Chauvin kuikandamiza shingo yake kwa goti kwa karibu dakika 9.

“Kwa masikitiko, wahanga wengi wa matukio kama hayo hawakuangaziwa, kwa kuwa matukio yao hayakurekodiwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ili ulimwengu uyaone,” aliandika balozi Dieudonne Desire Sougouri kwenye barua hiyo. 

Kifo cha Floyd ambacho kilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kimeibua machafuko nchini Marekani na maandamano sehemu mbalimbali duniani.

“Maandamano yanayoshuhudiwa ulimwenguni ni ukosoaji wa kukosekana kwa usawa na ubaguzi unaowakumba watu weusi na kutoka mataifa mengine wanaoishi nchini Marekani,” barua hiyo imesema.

Rais wa baraza hilo, Elisabeth Tichy-Fisslberger Jumatatu ijayo anatarajiwa kutangaza mapendekezo ya siku ambapo mjadala huo utafanyika, vinginevyo kama kutaibuka upinzani. 

Lakini taarifa zinasema  uwezekano ni mkubwa wa kufanyika mjadala huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles