Soko kuu Beijing lafungwa baada ya kuwepo virusi

0
519
HNDJJ0 Departmen Store (shopping mall). In Pacific century Place,Beijing, China

BEIJING, CHINA

MAMLAKA  za mji mkuu wa China, Beijing jana zililifunga soko kuu la mji huo baada ya kugundulika visa saba vya maambukizi ya virusi vya corona katika kipindi cha siku mbili zilizopita. 

Shirika la Habari la China Xinhua, limeripoti kuwa soko la Xinfadi lenye wafanyabiashara 4,000 litafanyiwa usafi wa kuua vimelea baada ya wafanyakazi wake kupata maambukizi na kubainika kuwepo virusi vya corona kwenye eneo hilo.

 Mamlaka za mji huo zimeamuru pia wafanyakazi wote wa soko hilo kupimwa virusi vya corona pamoja na kuchukua sampuli zaidi za vyakula na mazingira ya soko ili kubaini uwepo wa virusi. 

Tume ya Taifa ya Afya nchini China imethibitisha kugundulika visa hivyo vya maambukizi ambavyo ni vya kwanza katika mji huo mkuu katika kipindi cha siku 50 zilizopita.

Wakati huo huo Serikali ya Ufaransa imesema kuwa nchi hiyo itaendelea kufungua mipaka yake hatua kwa hatua kwa mataifa yaliyo katika kanda ya Schengen kuanzia Julai Mosi. 

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na mawaziri wa mambo ya ndani na wa mambo ya kigeni imesema uamuzi huo utazingatia hali ya mataifa mengine ya kanda hiyo pamoja na mwongozo ulioridhiwa na Umoja wa Ulaya. 

Siku ya Alhamisi, Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza kusogeza mbele mipango ya kulegeza vizuizi vya kusafiri katika kanda hiyo kutoka Juni 15 hadi mwanzoni mwa mwezi ujao. 

Lengo ni kudhibiti safari zisizo za lazima katika kukabiliana na kuenea kwa janga la virusi vya corona ambalo limewauwa zaidi ya watu 29,000 nchini Ufaransa.

Imeripotiwa kuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na mripuko wa virusi vya corona nchini Brazil imepindukia zaidi ya 40,000 katika kipindi ambacho pia maambukizi yamefikia watu zaidi ya 800,000. 

Taifa hilo linaloongoza kwa idadi ya vifo katika eneo la Amerika ya Kusini limerekodi vifo 1,239 katika kipindi cha masaa 24, na hivyo kuifanya idadi jumla ya vifo kupindukia 40,900. 

Hivi sasa Brazil inashika nafasi ya tatu kwa wingi wa vifo duniani, ambapo takwimu za jana ziliashiria kuipita Uingereza. 

Brazil yenye jumla ya maambukizi 802,800 inashika nafasi ya pili kwa maambukizi hayo baada ya Marekani.

Kwa mujibu wa makusanyo ya takwimu za shirika la habari la Uingereza Reuters zaidi ya watu milioni 7.43 wameripotiwa kuambikizwa virusi vya corona duniani kote na watu 416,755 wamekufa. 

Hadi sasa maambukizi yameripotiwa katika mataifa 210 tangu kuzuka kwake kwa mara ya kwanza Desemba nchini China.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here