25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Nyalandu atajwa kumvaa Lissu urais Chadema

ASHA BANI 

JOTO la kuwania kupeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye uchaguzi mkuu kwa nafasi ya urais, limezidi kupanda baada ya taarifa za kuwepo kwa makada maarufu wanaojiandaa kutangaza nia.

Mpaka sasa ni makada wawili tu ambao wameshatangaza nia ya kutaka ridhaa ya kuwania urais kwa tiketi ya Chadema ili kuchuana na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk John Magufuli.

Makada hao ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Kanda ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mchungaji Peter Msigwa.

Hata hivyo, habari za kuaminika zinaeleza kwamba, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, Lazaro Nyalandu, naye atatangaza nia yake mwishoni mwa wiki hii.

Kwa muda mrefu sasa, Nyalandu amekuwa akitajwa kuwa yupo kwenye mikakati mizito ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ili kupata nafasi ya kupeperusha bendera ya Chadema.

CHADEMA kilifungua milango kwa makada wanaotaka nafasi hiyo kutia nia kwa kuwasilisha taarifa rasmi kwa Katibu Mkuu kuanzia Juni 3 huku pazia likitarajiwa kufungwa Juni 15, mwaka huu.

Habari kutoka ndani ya CHADEMA zinaeleza kwamba, kutajwa kwa jina la Nyalandu kumezidi kuongeza joto la ushindani kutokana na aina ya siasa anazofanya tangu akiwa ndani ya CCM na hata alipotoka na kuhamia CHADEMA.

Habari zaidi kutoka ndani ya CHADEMA zinaeleza kuwa, Nyalandu amekuwa akishawisha na baadhi ya makada hasa vijana kutangaza nia huku mwenyewe akiwataka kusubiri muda ufike ndipo ataamua.

Baadhi ya makada wa CHADEMA wamelieleza Rai kwamba, kwa sasa mbali ya Lissu na Mwenyekiti wao Taifa, Freeman Mbowe, Nyalandu anatajwa kama mwanasiasa mwenye ushawishi kisiasa huku kudumu kwake katika siasa na kuhudumu kama Waziri kunampa nafasi ya kuwa mtu sahihi.

“Kama jamaa (Nyalandu) atatangaza nia basi kutaongeza chachu na kuwapa wanachama wakati mgumu kufanya uamuzi. Ana uzoefu na siasa za Tanzania na kubwa ni kuwa, amehudumia kama Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili hivyo, ni mzoefu wa ukweli. 

“Kwa waliotangaza nia mpaka sasa hakuna aliyewahi kuwa waziri ama naibu atakuwa Nyalandu peke yake, sasa nadhani hata CCM wenyewe hili litawatisha sana. Kutakuwa na upinzani mkali,” alisema kada huyo ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini.  

Kada mwingine, Mabula Christopher ambaye naye amekuwa akishawishi Nyalandu kutangaza nia, amedai kuwa ukomavu wake kisiasa ndio unaweza kuibeba Chadema katika kuikabili CCM.

“Napenda sana misimamo yake ndani ya CHADEMA, anafanya siasa safi na zisizo na chuki na hilo alilionyesha wakati wa uchaguzi wa ndani ya Chama. Hayumbi kwenye misimamo yake na anajua kusoma mazingira kwenye uwanja wa vita. Kulikuja wimbi kubwa la makada kutoka CCM waliohamia kwetu, lakini wote wamerudi walipotoka na Nyalandu ameendelea kuwepo hapa bila kuyumba,” aliongeza.

Kuhusu Lissu

Huyu ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), Tundu Lissu, aliyetangaza nia yake akiwa nchini Ubelgiji alipokwenda kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu Septemba 7, 2017 jijini Dodoma.

Pia, mwanasheria mkongwe na amewahi kuwa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA kwa vipindi viwili. Amepata kuwa Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mchungaji Msigwa

Ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa vipindi viwili mfululizo na pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa CHADEMA na Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.

Kuhusu Nyalandu 

Kwa sasa ni Mwenyeketi wa Kanda ya Kati CHADEMA na Mjumbe wa Kamati Kuu. Pia, anaongoza nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Mahusiano Mtambuka ya Kamati Kuu ya CHADEMA. 

Nyalandu amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili naa Utalii, na pia Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda katika katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Amekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM kuanzia mwaka 2000 na kuchaguliwa kwa vipindi vinne mfululizo na Oktoba mwaka 2017 alipojiuzulu Ubunge na Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na kujiunga na CHADEMA. 

Nyalandu alikuwa mstari wa mbele katika kusaidia Jamii katika masuala  ya elimu na afya, ambapo alikuwa Mwanzilishi Mwenza wa Shirika la STEMM ambalo limesomesha wanafunzi zaidi ya 10,000 kwa kuwalipia ada za Sekondari na ufadhili katika vyuo vikuu. 

Nyalandu ana shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Buckingham, England, na  alisoma digree ya Awali Waldorf University, USA, na Chuo Cha Wartburg, USA. Alihitimu elimu ya Sekondari ya Wanafunzi wenye Vipaji Maalumu Kibaha, Pwani, na Ilboru, Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles