23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Madhara ya corona kupunguza ukuaji pato la taifa – Dk. Mpango

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philp Mpango, amewasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 ikionyesha ukuaji wa pato halisi la taifa unatarajiwa kupungua kutoka makadirio ya asilimia 6.9 na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019.

Dk. Mpango alisema hali hiyo ni kutokana na athari za ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wakubwa wa kibiashara wa Tanzania.

Alisema shabaha ya malengo ya uchumi wa juu kwa mwaka 2020/21 ni kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia tatu hadi tano kwa mwaka 2020/21 na mapato ya ndani kufikia asilimia 14.7 ya pato la taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0 mwaka 2019/20.

Dk. Mpango alisema matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya pato la taifa mwaka 2020/21 na nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada kuwa asilimia 2.6 mwaka 2020/21 ikiwa ni chini ya asilimia 3.0.

Alisema shabaha nyingine ni akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.0.

Dk. Mpango alisema pia mwaka huu nchi imepata mvua nyingi zilizosababisha uharibifu wa miundombinu, hivyo  mwaka 2020/21, Serikali itaweka kipaumbele katika ukarabati wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii iliyoharibiwa na mvua, ikijumuisha barabara na madaraja, reli, nguzo za umeme, mabwawa ya maji na majengo ya taasisi za afya na elimu.

Alisema Serikali imetenga Sh trilioni 12.90, kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2020/21.

 “Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 10.16 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.74 ni fedha za nje. Kiwango kilichotengwa kinaendana na lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano la kutenga kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Dk. Mpango.

MWAKA 2019

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango alisema pato halisi la taifa lilikua kwa asilimia 7.0 mwaka 2019 kama ilivyokuwa mwaka 2018.

“Ukuaji huu ulitokana na kuendelea kuimarika kwa sekta ya madini, kuboreshwa kwa huduma za usafiri na usafirishaji, pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, miradi ya nishati ya umeme pamoja na ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema Dk. Mpango.

Alisema sekta zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji mwaka 2019 ni pamoja na madini iliyokua kwa asilimia 17.7, ujenzi (asilimia 14.8), sanaa na burudani (asilimia 11.2), na usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 8.7).

PATO LA MTU MMOJA MMOJA JUU

Dk. Mpango alisema  mwaka 2019, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu 54,265,158 na pato la wastani la kila mtu lilifikia Sh 2,577,967 kutoka Sh 2,452,406 mwaka 2018, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 5.1.

Alisema kiasi hicho cha pato la wastani kwa kila mtu kwa mwaka 2019 ni sawa na dola za Marekani 1,126.4 ikilinganishwa na dola za Marekani 1,083.2 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 4.0.

MAKUSANYO YA NDANI

Dk. Mpango alisema katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, makusanyo ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri, yalifikia Sh trilioni 16.075  sawa na asilimia 92.5 ya lengo la Sh trilioni 17.375.

Alisema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.2 ikilinganishwa na Sh trilioni 14.071 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

Dk. Mpango alisema mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalifikia Sh trilioni 13.465 sawa na asilimia 94.7 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 14.224.

“Kiasi kilichokusanywa ni sawa na ongezeko la asilimia 14.9 ikilinganishwa na Sh trilioni 11.720 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19. 71,” alisema Dk. Mpango.

Alisema Julai 2019 hadi Machi 2020, makusanyo ya maduhuli yalifikia Sh trilioni 2.071 ikilinganishwa na lengo la Sh trilioni 2.576 sawa na asilimia 80.4 ya lengo.

Aidha, hadi Machi 2020, alisema mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yalikuwa Sh bilioni 538.6, sawa na asilimia 93.7 ya lengo la Sh bilioni 575.3.

MATUMIZI

Dk. Mpango alisema katika mwaka 2019/20, Serikali iliendelea kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya matumizi hususan katika miradi ya maendeleo.

Aidha, alisema Serikali iliendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia kuongezeka kwa malimbikizo ya madai.

“Vile vile, Serikali iliendelea kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yenye kuchochea ukuaji wa uchumi, lengo kuu likiwa ni kuwa na matumizi bora ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya fedha.

“Ili kutimiza azma hiyo, sera za matumizi zililenga kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20 wenye maeneo makuu manne ya vipaumbele, ambayo ni viwanda na kilimo, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, na ufuatiliaji na tathmini,” alisema Dk. Mpango.

Alisema katika mwaka 2019/20, Serikali ilikadiria kutumia Sh trilioni 33,105.4 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 20,856.8 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.0 ya bajeti na kiasi cha Sh trilioni 12.248.6 kilitengwa kwa matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37.0 ya bajeti.

Aidha, Dk. Mpango alisema katika bajeti ya fedha za maendeleo, kiasi cha Sh trilioni 9.737 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.510 fedha za nje.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles