Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Jumanne Juni 9, amemtembelea na kumjulia hali Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika Hospitali ya Ntyuka jijini Dodoma kabla hajatolewa na kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Majaliwa amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za tukio la kuvamiwa kwa kiongozi huyo na kumuombea uponyaji wa haraka wa majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu ambao bado hawajajulikana wakati akiingia nyumbani kwake jijini Dodoma usiku wa kuamkia leo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za tukio la kuvamiwa kwa Mheshimiwa Mbowe na watu ambao bado hawajajulikana, ninamuomba Mwenyezi Mungu amjalie apone haraka ili aweze kurejea katika majukumu yake,” amesema Mbowe.
Baadhi ya wabunge wa upinzani waliokuwepo hospitalini hapo na ambao walimpokea Waziri Mkuu ni Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.