24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Tatoa yashtukia hujuma uchumi wa Taifa

CHRISTINA GAULUHANGA Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), kimeshtukia hujuma za uchumi zinazofanywa na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, kimeiomba Serikali kukaa kikao cha pamoja na wadau wa malori ili kujadili changamoto zinazowakabili mipakani na kusababisha shughuli kusimama mara kwa mara.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa TATOA, Elias Lukumay alisema sekta ya usafirishaji kwa njia ya barabara ni moja ya eneo ambalo limeota vikwazo hasa mipakani jambo ambapo linachangia kuyumba kibiashara.

Alisema yapo mambo manne ambayo yanawafanya washindwe kufanya shughuli zao kwa wakati, ikiwamo unyanyasaji na unyanyapaa kwa madereva wa Tanzania, gharama za ufanyaji biashara kutokuwapo kwa usawa wa ufanyaji biashara na vyeti vya vipimo vya Covid 19 vinavyotolewa kwa madereva mipakani.

“TATOA inatambua juhudi kubwa na za haraka ambazo Serikali imezichukua kufikiwa makubaliano ya kurejeshwa kwa huduma katika mipaka ya Tunduma, Horohoro,  Namanga na Rusumo ambapo Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto ilianzisha vituo vya kupima madereva na kusaidia kuondoa sintofahamu iliyokuwapo awali,” alisema Lukumay.

Alisema kabla ya hapo wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Corona unaosababishwa na virusi vya Covid-19,  madereva walikuwa wakisoteshwa mipakani na kudaiwa baadhi yao wana virusi vya ugonjwa huo.

Lukumay akifafanua vitendo hiyo na kusema madereva wao wananyanyasika na kunyanyapaliwa katika mipaka ya Rwanda na Namanga nchini Kenya.

“Madereva hawa wamekaa muda mrefu Rusumo, wakisubiri kushusha mzigo katika eneo ambalo halina huduma muhimu toshelezi za kijamii kwa madereva wanaosubiri kuvuka na hata wale wanaovuka kwa utaratibu kuingia Rwanda kwa utaratibu uliowekwa wa ‘escort’, bado wanapitia mazingira magumu ya kukosa huduma za kijamii wakiwa chini ya escort,” alisema Lukumay.

Alisema kwa utaratibu wa sasa gari za hapa nchini zinatakiwa kuishia mipakani, isipokuwa kwa zile zilizobeba mizigo iliyoainishwa kama bidhaa muhimu.

Alisema TATOA pamoja na makubaliano yaliyofikiwa bado kuna mambo yameendelea kujitokeza na  kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana.

Aliyataja huku, akiiomba serikali iweze kuingilia kati ili yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Alisema wapo madereva ambao wamekaa muda mrefu katika mpaka wa Rusumo,wakisubiri kushusha mzigo na wengine wakisubiri kuvuka kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Wakati haya yakiendelea kwa madereva wetu, gari za Rwanda zinaruhusiwa kusafiri zaidi ya kilometa 1,000 kuja Dar es Salaam kuchukua mizigo bila bughudha yoyote na kupeleka mizigo hiyo hadi kwa wateja mlangoni.

“Utaratibu huu, umesababisha waagizaji mizigo kupendelea zaidi  kutumia magari ya Rwanda, yanawapelekea hadi mlangoni wakati ya Tanzania yanashusha mpakani, kufanya mazingira ya biashara kutokuwa sawa kwa pande zote mbili,” alisema Lukumay.

Mwenyekiti wa TATOA, Angelina Ngalula, alisema   gharama zilizotengwa na Serikali ya Rwanda kuna miundombinu hafifu ya ushushaji ,uhudumiaji na uhifadhi mizigo na kusababisha magari ya Tanzania kusubiri muda mrefu mpaka pale yanapopatikana magari ya Rwanda kufaulisha mzigo.

“Ucheleweshwaji huu unasababisha wasafirishaji wa Tanzania kuendelea kutozwa faini ya makontena hadi shilingi  120,000 kwa siku kwa kontena moja kwa kuchelewesha kurejesha kontena tupu kwa wenye meli kwani kontena hizo ni mali za wenye meli na ni wajibu msafirishaji au wakala wa forodha kurudisha kwa muda uliokubaliwa,” alisema.

Alisema wanachama wa TATOA wapo katika wakati mgumu unaoweza kusababisha kufilisika kwa sababu ya gharama za tozo zinazosababishwa katika mpaka wa Rwanda.

Akizungumzia kuhusu vyeti vinavyotolewa kwa madereva vya Covid-19, alisema makubaliano yalifikiwa hivi karibuni na Kenya ilikuwa ni madereva kupima na kupata cheti ambacho kingekubalika pande zote mbili.

Alisema cheti hicho kingemwezesha dereva kupita bila vikwazo pamoja na makubaliano hayo mamlaka za Kenya zimebadili makubaliano ghafla na kuvikaa vyeti hivyo bila taarifa, madereva kuendelea kupata taabu katika mpaka wa Namangan a kusababisha hasara kwa wafanyabiashara hasa wanaosafirisha bidhaa zinazoharibika haraka.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), Tonny Swai alisema wanaomba wakae meza ya mazungumzo kabla hawajaharibikiwa.

Alisema kwa sasa kuna changamoto  ya malori kuchelewa kupita kwakuwa yanakaa muda mrefu na kusababisha baadhi ya kampuni kufilisiwa.

Alisema mawakala wa forodha wanakumbana na gharama za uhifadhi wa makasha na gharama za ucheleweshaji wa kurejesha makasha kwa wenye meli kuwa kubwa kwa sababu ya kuchelewa mipakani.

“Tunaiomba Serikali iunde tume maalum  ishirikiane na wadau kushughulikia jambo hili  ili jambo hili liweze kumalizwa,”alisema Swai.

Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta waliwaagiza mawaziri wa uchukuzi na wakuu wa mikoa iliyopo katika pande zote za mpaka wa Tanzania na Kenya kukutana na kutatua mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa malori ya mizigo kuvuka mpaka huo .

Hata hivyo, madereva wa malori wameendelea kusota mipakani kwa muda mrefu mbali ya uwapo wa makubaliano hayo.

Ikumbukwe Tanzania na Kenya, zimekuwa kwenye mvutano,siku chache zilizopita umeibuka mgogoro katika vituo vya mpaka wa Tanzania na Kenya katika mikoa ya Mara, Tanga, Arusha na Kilimanjaro baada ya malori ya mizigo ya kutoka Tanzania kuzuiwa kuingia Kenya kwa madai ya madereva wanaopimwa kukutwa na corona.

Awali Kenya ilikuwa ikiwatuhumu madereva wa malori yanayotoka Tanzani kuwa wana maambukizi ya virusi vya corona hatua ambayo ilipekea kufunga mpaka wake, kabla ya Tanzania kujibu mapigo hayo.

KAULI  YA SERIKALI

MTANZANIA ilimpomtafuta Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema  wanasubiri hoja za TATOA ziwasilishwe kwa maandishi mezani kwake ndipo waweze kutoa msimamo wa serikali.

“Wakishaleta hoja zao mezani, serikali itazipitia na kuangalia mahali ambapo panahitaji kutolea tamko tutafanya hivyo kwa haraka zaidi,” alisema Kamwelwe.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles