Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
MPANGO wa Taifa wa Damu Salama, umesema katika kipindi hiki cha mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona(Covid-19),umeweka mikakati maalumu ya ukusanyaji damu ili kuepuka maambukizi
Kutokana na hilo, mpango huo unatoa wito kwa Watanzania kijitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, wakati wa mahojiano maalumu kuelekea maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu duniani Juni 14,Meneja wa Mpago wa Damu Salama kanda ya Mashariki,Dk. Avelina Mgasa alisema hivi sasa kuna uhitaji mkubwa wa damu, wanaendelea kuhamasha jamii iendelee kuchangia damu.
“Kiwango cha uchangiaji damu kimeshuka kutoka chupa 31,502 za mwezi Februari,chupa 25,737 za Machi hadi kufikia chupa 22,044 Aprili,hali hiyo imechangiwa na shule na vyuo kufungwa hivyo kukosa fursa za kukusanya damu katika ofisi mbalimbali.
“Kingine ambacho kimesababisha ukasanyaji wa damu kuwa mdogo ni zuio la mikusanyiko kutokana na maelekezo ya serikali katika kupambana na Covid-19 kwani maeneo hayo ndiyo yamekuwa yakitegemewa zaidi,”alisema.
Alisema hivi sasa wamejipanga kuhakikisha watu wanachangia damu katika mazingira salama ambayo yatawawezesha kujikinga na Covid-19.
“Kutokana na hilo basi uhitaji wa damu ni mkubwa sisi kama damu salama tumejipanga, kwani uchangia wa damu ni tendo salama na mpango umeweka mikakati mbalimbali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona katika vituo vya kuchangia damu.
“Tumuweka maji tiririka na sabuni kwaajili ya kunawa mikono,vitakasa mikono,vifaa kinga kwa watumishi kama barakoa, apron/koti, gloves, na goggles,thermo scanner kwaajili ya kupima jotoridi la mwili kwa kila mchangia damu.
“Tunatakasa vitanda na vifaa vinavyotumika na wachangia damu,mpangilio unaozingatia umbali kati ya mtu na mtu (social distance) hivyo tahadhari zote zitazingatiwa watu wajitokeze kuokoa maisha ya wenzao,”alisema.
Alisema mwaka huu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsi,Wazee na Watoto ,Ummy Mwalimu, atazungumza na wananchi na kuwashukuru wachangia damu.
Kaulimbili katika maadhimisho hayo, ni Damu Salama Inaokoa Maisha.
Mwisho