29.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Ndalichako atuma salamu shule za kidato cha sita ambazo walimu hawajaripoti

Na BRIGHITER MASAKI -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amewaagiza wamiliki wa shule binafsi kumaliza tofauti zao na walimu ili wanafunzi wa kidato cha sita wapate haki yao ya elimu na kumaliza mitihani yao salama.

Akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu baadhi ya shule ambazo walimu wake hawajaripoti licha ya kufunguliwa kwa kidato cha sita, Ndalichako alisema  changamoto za kielimu kati ya mmiliki wa shule na mwalimu zisiathiri taaluma ya wanafunzi.

Ndalichako alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa kupokea na kukabidhi matanki 100 kutoka Kampuni ya Africab.

Alisema swala la mikataba baina ya mwajiri na mwalimu Serikali haiwezi kuingilia.

“Mikataba baina ya mwajiri na mwalimu, Serikali haiwezi kuingilia, ina wajibu wa kufuatilia vigezo na masharti, ambavyo vimewekwa vinatakiwa kufuatwa ili wanafunzi wapate taaluma stahiki.

“Swala la walimu shule binafsi kutoripoti mashuleni nimechukua na nitalifuatilia, kwa kuwa sijapata taarifa rasmi nitalifuatilia zaidi ila kuna vigezo vya kuwa na shule binafsi.

“Shule inavyosajiliwa inatakiwa kukidhi vigezo na masharti ya Wizara ya Elimu, moja ya sharti ni kuwa na walimu wa kutosha kuwapa taaluma wanafunzi, kwa kuwa wamerejea mashuleni wanatakiwa kupata elimu,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliongeza kuwa shule na vyuo wamelipokea kwa kasi suala la tahadhari dhidi ya kujikinga na maambukizi kwa walimu na wanafunzi pamoja na taasisi kufuata maagizo ya Wizara ya Afya.

Kuhusu matanki aliyokabidhiwa na Kampuni ya Africab, alisema yatapelekwa shule za sekondari 67 pamoja na vyuoni, ili kupambana na kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

“Wizara ya Afya wametoa maelekezo jinsi ya kufanya kazi na kujikinga na ugonjwa wa corona kwa kunawa mikono na maji tiririka pamoja na kupaka sanitizer na kuvaa barakoa.

  “Nimepokea na kukabidhi matakti 100 kwa walimu wakuu, yatakayosaidia shule za sekondari na vyuo kujikinga na maambukizi ya corona,” alisema Profesa Ndalichako.

Aidha aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kusaidia kwenye maeneo mbalimbali ili kuzidi kusaidia wanafunzi wanaporejea mashuleni waweze kupata elimu bora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Africab  inayojishughulisha na kutengeneza vifaa vya umeme, Mohammed Ezzi, alisema kuwa ni wakati wa kurudisha shukrani kwa jamii kupitia wanafunzi.

 “Yote haya ni kupambana na homa kali ya mapafu ya Covid-19, tunashukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupa fursa na kuwataka Watanzania kutumia bidhaa za ndani, hii ndiyo maana kubwa ya Tanzania ya viwanda. 

“Tumetoa matanki 100 yenye thamani ya Sh milioni 50 yatakayosaidia wanafunzi kupata elimu iliyo bora huku wakijikinga na maambukizi ya corona,” alisema Ezzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles