Dk. Chaula azitaka taasisi za umma kutumia Posta kusafirisha vifurushi

0
1064

Mwandishi wetu -Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dk. Zainab Chaula, amezitaka taasisi za Serikali kutumia huduma za Shirika la Posta Tanzania (TPC) kusafirisha bidhaa, vifurushi na vipeto kwa usalama zaidi.

Dk. Chaula aliyasema hayo wakati wa kikao cha menejimenti ya wizara yake na viongozi wa TPC wakiongozwa na Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang’ombe.

Kikao hicho kilifanyika jana kwenye ukumbi wa wizara hiyo uliopo Mtumba, Dodoma.

Shirika hilo lilifika ofisini hapo kwa lengo la kujitambulisha na kuwasilisha taarifa yake.

Dk. Chaula alisema TPC imepewa dhamana kisheria kuwa msafirishaji mkuu wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa mbalimbali kwa mujibu wa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na. 19 ya mwaka 1993 iliyoanzisha shirika hilo na ni shirika la umma ambalo Serikali imewekeza.

Alisema TPC imefanya kazi kubwa ya kusafirisha sampuli kutoka hospitali mbalimbali nchini kwenda Maabara Kuu ya Serikali wakati wa janga la corona pamoja na kusafirisha nyaraka za mahakama zote nchi nzima, benki, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mifuko ya hifadhi za jamii, hisa za kampuni mbalimbali na kutumia usafiri wa ndege kwenda ndani na nje ya Tanzania.

Aliitaka TPC kuunganisha huduma za Posta na anwani za makazi na postikodi na simu za mkononi ili kuhudumia wananchi katika kufanikisha azma ya Serikali ya kurahisisha na kufanikisha usambazaji na usafirishaji wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa kwa wananchi.

“Tunataka mwananchi afikishiwe nyanya nyumbani kwake na sio atumie pikipiki kuzunguka kwa muda mrefu na kupiga simu bila kufika kwa mteja kwa wakati,” alisisitiza Dk. Chaula.

Naye Posta Masta Mkuu wa TPC, Mwang’ombe aliziomba taasisi za Serikali kutumia shirika hilo kusafirisha barua, vifurushi na vipeto kwa kuwa bidhaa zao zitafika kwa usalama na uhakika kwa kuwa linatumia huduma ya mtandao wa Tehama kutoa huduma zake kwa wateja kwa kuunganisha ofisi zake 202 zilizopo maeneo mbalimbali nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Jim Yonazi alishauri shirika hilo kuwa pamoja na kuboresha huduma zake ndani ya nchi, pia amelitaka kufungua milango yake na kufanya biashara na nchi nane za jirani zinazopakana na Tanzania.

Amelitaka kuongeza huduma za lojistiksi kwenda nchi za jirani za usafirishaji wa bidhaa, biashara mtandao, uwakala na maduka ya kubadilisha fedha ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti mara kwa mara ili kuendeleza biashara zake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here