27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kairuki awataka wawekezaji kuwasilisha taarifa TIC

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji, Angellah Kairuki, amewataka wawekezaji waliosajili miradi yao Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuwasilisha taarifa za maendeleo na changamoto zao kila baada ya miezi sita ili ziweze kufanyiwa kazi za uboreshaji na utatuzi wa changamoto zake kwa wakati.

Kairuki amesema kanuni za usajili za TIC zinawataka wawekezaji hao kufanya hivyo na kwamba hatua hiyo inalenga kuwaweka karibu wawekezaji hao ambao wamekuwa na tija ya kiuchumi kutokana na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani na kilimo ambazo hutoa ajira kwa Watanzania na ulipaji kodi unaostahili.

Aliyasema hayo hivi karibuni  alipotembelea Kiwanda cha OK Plast Limited kilichopo Vingunguti, Dar es Salaam kinachochakata bidhaa (vyuma) chakavu na kuzalisha rodi za shaba, nyaya za umeme, betri ingots na mikeka ambacho kimeajiri wafanyakazi 595 wa kitanzania na raia wa kigeni watano.

“Nawasihi wawekezaji wote mliojisajili na TIC pelekeni taarifa zenu za maendeleo ya miradi yenu kila baada ya miezi sita ili tujue ni wapi kuna changamoto tuweze kuzitatua kwa wakati, ni kwa nia njema sana, Serikali yenu ipo na ni sikivu.

“Pia naomba niwapongeze wamiliki wa kiwanda hiki cha OK kwa ulipaji wa kodi mzuri na mmeajiri Watanzania wengi, na wengine igeni mfano wa kiwanda hiki,” alisema Kairuki.

Meneja wa kiwanda hicho, Fadil Ghaddar alisema uwekezaji wao kwa sasa umefikia Sh bil 10 na kwamba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005 wamepata mafanikio makubwa, ikiwepo soko la uhakika la ndani ya nchi pamoja na baadhi ya nchi jirani ikiwemo Kenya.

Mbali na uzalishaji wa bidhaa hizo, kiwanda hicho pia kinatoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za metali kwa vijana waliowaajiri ili kuwajenga kiuchumi kwa kuanzisha viwanda vyao pindi wanapoamua kuacha kufanya kazi kiwandani hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles