30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kalemani ateta na wakandarasi REA

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amekutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza na kujadiliana maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa nchini kote.

Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Zena Said, Naibu Katibu Mkuu, Leonard Masanja, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo pamoja na wajumbe wa bodi hiyo.

Wengine ni Kaimu Kamishna wa Nishati, Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Amos Maganga na menejimenti yake, mameneja wa Tanesco wa kanda pamoja na wasimamizi wa mradi husika kutoka wizarani.

Akifungua kikao, Dk. Kalemani aliwapongeza wakandarasi hao kutokana na kazi wanayoifanya ya kusambaza umeme vijijini, lakini amebainisha msimamo wa wizara kuwa haitarajii kuongeza muda, hivyo amewataka kuongeza bidii na ubunifu ili waweze kukamilisha kazi ifikapo Juni 30, kama ilivyoainishwa katika mkataba.

“Pamoja na kwamba wengi wenu mnafanya kazi nzuri, lakini wapo wachache ambao wanasuasua. Ninawataka mjipime kutokana na utendaji wenu kama mtastahili kuendelea na kazi nyingine zitakazofuata,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema kuwa kamwe wizara haitaingia mikataba mipya ya kazi na wakandarasi wababaishaji, huku akisisitiza kuwa ni wale tu wanaofanya vizuri katika miradi ya sasa ndio watakuwa na nafasi ya kupewa kazi nyingine.

Katika hatua nyingine, Dk. Kalemani aliwataka wakandarasi hao kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma, hivyo kufanya kazi kwa weledi na uzalendo huku wakizingatia masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla kwani ndivyo watumishi wa umma wanavyopaswa kuwa.

Alifafanua kuwa mtumishi wa umma ni yeyote aliyeajiriwa au kuingia mkataba na Serikali kufanya kazi fulani na ataendelea kuwa na sifa hiyo hadi pale mkataba wake unapokoma.

Aidha, alitoa pongezi za pekee kwa wakandarasi ambao hadi sasa wamekamilisha kazi kwa asilimia nyingi, huku wakiwa na uelekeo wa kukamilisha muda mfupi kutoka hivi sasa.

Wakandarasi hao wametajwa kuwa ni Steg International Ltd anayetekeleza mradi katika mikoa ya Mbeya na Songwe, Sengerema Engineering Group Ltd (Iringa), Derm Electrics (T) Ltd (Tanga) na Nakuroi Investment Co. Ltd (Rukwa).

Vilevile, Dk. Kalemani ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi wa REA kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia miradi husika na pia aliipongeza menejimenti ya wakala huo na watumishi wake wote huku akiipambanua kwamba imetengeneza historia Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles