32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Simulizi ya kusisimua aliyepona corona na mkewe

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

‘KUNA mambo usiombe yakukute, yasikie tu kwa jirani’ usemi huu unaweza kuwa na maana kubwa kwa Deogratius John Senya Mkazi wa Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam ambaye yeye na mkewe, Silvia Kimaro walifikwa na janga linalotikisa dunia kwa sasa la corona.

Senya yeye alipona kwa kujifukiza, lakini kwa mkewe ambaye alikuwa mjamzito hali ilikuwa ni tofauti kwani hadi kupona kwake na hata kuokoa maisha ya kiumbe kilichokuwa tumboni amepitia misukosuko mikubwa ambayo sasa imewafanya wabaki na madeni ya mamilioni baada ya matibabu yake kugharimu zaidi ya Sh milioni 50.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana baada ya mkewe kutoka hospitali juzi, Senya ambaye ni mjasiriamali mdogo katika eneo la Kariakoo, mwenye kipato cha kati anasimulia jinsi alivyoambukizwa corona na mtu aliyefika dukani kwake na kisha yeye kumuambukiza mkewe aliyekuwa na ujauzito wa wiki 36.

Alisema yeye baada ya kuugua na kushindwa kupata nafuu hata baada ya kufika hospitalini kabla ya baadae kupona kwa kujifukiza, wiki mbili baadae mkewe alianza kuumwa.

Senya alisimulia jinsi alivyohangaika hospitali sita ili kuokoa maisha ya mkewe aliyegundulika na kuwa na virusi vya corona.

Kwa mujibu wa Senya alimpeleka mkewe katika hospitali binafsi ambako aliambiwa ana malaria moja na hata baada ya kupewa dawa hali yake ilizidi kuwa mbaya.

“Aprili 18, mke wangu alianza kujisikia vibaya mwili wake ulichoka akaenda kituo cha afya Tabata Shule wakampa dawa za malaria lakini kadri siku zilivyokwenda mbavu na kifua zilimbana.

“Nilivyoona hali inakuwa mbaya nikampeleka hospitali binafsi wakampima walisema ni malaria wakamchoma sindano ya kwanza lakini alivyorudi ya pili alizidiwa akashindwa kupumua wakamchoma sindano mbili,”alieleza Senya.

Alisema baada ya kupata matibabu hayo pia hakuweza kupata nafuu badala yake aliendelea kuzidiwa hali iliyofanya afikirie kumpeleka hospitali kubwa zaidi.

“Aprili 22 alizidiwa usiku kama saa tano tukamchukua nikatoka naye sikutaka kumpeleka hospitali ya mwanzo nikampeleka hospitali kubwa na tulivyofika alipokelewa na daktari akamwona lakini baada ya kuhoji na kumchunguza mgonjwa dakatri alitoka nje.

“Alituambia tusubiri atarudi alivyoondoka tu akaja mhudumu akawa anapulizia ‘sanitizer’ kwenye chumba nikashtuka nikasema labda atakuwa na corona.

“Baada ya kufikiri hivyo hali ilibadilika ambapo wahudumu wakatutenga ghafla ndio nikajua hapa kuna shida, hata hivyo baadae daktari akaniambia kuwa mke wangu anahitaji kuwekewa oksijeni hivyo hospitali yao haina, nikafikiria kuwa ile ni hospitali kubwa nikajiuliza ni kweli hawana oksijeni? hata hivyo sikuwa na la kufanya ,”alibainisha

Alisema baada ya hapo alianza safari nyingine ya kutafuta matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Temeke , hata hivyo juhudi zake ziligonga mwamba baada ya kuambiwa aende hospitali ya Rufaa ya Amana .

“Nilivyofika Amana ilikuwa saa sita usiku nako wakaniambia hawapokei wagonjwa ambao hawana rufaa kutoka katika kituo cha afya huku hali ya mke wangu ikizidi kuwa mbaya ,”alisema Senya.

Alisema baada ya kupewa majibu hayo akaamua kurudi tena kufata utaratibu wa rufaa huku mgonjwa akiwa ameanza kupata shida ya kupumua na hali yake ya ujauzito.


Silivia Kimaro (kulia) akifurahia na mtoto wake baada ya kutoka hospitali akiwa amepona corona.

“Nilivyorudi kituo cha afya daktari akaniambia hatuwezi kumpokea hapa kutokana na hali yake kuwa mbaya hivyo akasema aende hospitali ya Wilaya ya Ilala, tulivyofika tukapokelewa na kuandikiwa kumwona daktari ambaye alitupokea vizuri na kutuhudumia kwa haraka .

“Vipimo vilifanyika haraka katika hospiali ya Ilala ikiwemo vipimo vya ultrasound, damu baadae majibu yalionesha kuwa mgonjwa alikuwa amejaa maji kwenye mapafu, yule dakatari aliendelea kuhangaika kuhakikisha anapata huduma nzuri na nampongeza aliweza kutumia nafasi yake ipasavyo.

“Kutokana na hospitali hiyo kutokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa isipokuwa waliojifungua daktari akashauri tutafute gari la wagonjwa ili apelekwe hospitali ya Temeke baada ya kusubiri kwa saa nne asubuhi tukaambiwa gari lilipata ajali na wakasema kama tuna gari binafsi tumpeleke ikabidi aende kwa gari langu,”alisema.

Baada ya kufika Hospitali ya Temeke kwa mara ya pili licha ya mgonjwa kuwa na hali mbaya alisema walilazimika kufuata utaratibu wa kupanga foleni hadi walipofikia huduma

“ Hata ilipofika zamu yake mgonjwa wakamweka pembeni wakajadili, madaktari wakasema apelekwe Muhimbili kutokana na hali yake kuwa mbaya, hata hivyo walivyopiga simu huko walijibiwa hospitali haipokei wagonjwa wa dharura, wakafanya mazungumzo ya muda mrefu ndio wakakubaliana .

“Alivyofika Muhimbili saa tisa jioni akapelekwa wodi ya wazazi ambako hadi saa kumi na moja jioni alikuwa hajapata huduma yoyote na alikuwa anaendelea kuzidiwa akawa haongei tena nivyokuwa nawauliza manesi kwanini hawamuhudumii wakasema madaktari wanakuja.

“Hadi saa nne usiku, walikuwa wanasubiri watu wa maabara waje kuchukua vipimo, mke wangu sasa hata rangi ikabadilika akawa mweupe hadi macho, haongei tena nikijaribu kuwashawishi ahudumiwe wahudumu wakasema hawawezi kumuhudumia na wanasubiri maelekezo na pia hawana vifaa vya kukinga .

Alisema kutokana na hali hiyo mkwe wake alikata taamaa kabisa na kuongea kwa sauti ya chini kuwa wamefikia mwisho wa kupambania uhai wake.

“Nikatoka nje nikawauliza wahudumu kuwa hakuna hospitali inayoweza kumpokea hata binafsi nikawaza kuwa inawezekana Aga Khan.

“Nikaamua niende kujaribu Aghakan, nilipomwomba mgonjwa wangu nimpeleke ninakokujua mimi walikuwa wanakataa wanasema wanasubiri vipimo nikawaambia huyu ni mke wangu nikasaini nikamchukua nikampeleka Aga Khan.

MATIBABU YA AGA KHAN

Baada kufika Aghakahn mkewe alipokelewa na kuanza kupatiwa huduma haraka zaidi.

“Daktari alihoji sababu za kumwacha mgonjwa hadi akazidiwa hivyo, nikamwambia nimezunguka naye sana nikaona nije hapa mara ya mwisho, timu ya madaktari walimpokea wakamuhangaikia mara moja.

“Baada ya hapo wakaniita wakasema kutokana na hali yake kuzidiwa oksejeni ya kawaida haiwezi kumsaidia wakashauri awekewe ventilator, ambapo walinitaka nisaini kwa sababu huwa ina madhara.

“Wakati huo nilikuwa na Sh. 17,000 mfukoni nilivyotoka nyumbani nilikuwa na Sh 300,000 ambayo

nyuma ya pazia nilimalizia kwenye mizunguko ya hospitali,” alisema.

Alisema akili ilipomkaa sawa akashtuka kwamba amempeleka mkewe kwenye hospitali ya gharama ilihali akiwa hana fedha ya kutosha japo hilo halikumkatisha tamaa.

Alisema Aga Khan waliendelea kumuhudumia pasipo kudai gharama yeyote.

“Waliniambia na mtoto aliyekuwa tumboni alianza kuathirika hata hivyo wakasema wanapambana kuwasaidia wote, ilipofika asubuhi wakaniambia wamefanikiwa kumtoa mtoto na yuko salama kabisa isipokuwa mama yake yuko Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).

GHARAMA ZA MATIBABU

Senya alisema mkewe alikaa ICU kwa siku 19 hivyo hakujua gharama ya matibabu itakuwa kiasi gani.

“Aprili 25 wakanipigia simu wakasenma wanahitaji kiasi cha milioni tatu, nikawapa kwasababu kwanza nilikuwa na furaha sana.

“Baadae nikaambiwa siruhusiwi kumwona mke wangu ICU na walinipigia simu kwamba gharama za matibabu zimefika Sh. milioni 50.87

“Alikaa hospitali siku 26 kati ya siku hizo 19 alikuwa ICU jana nililipa Sh milioni 31.13 gharama ya mtoto ni milioni mbili kasoro.

Alisema kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa ameuza viti vingi na pia amekopa fedha kutoka kwa watu mbalimbali.

“Aga Khan waliniambia hadi Jumanne wiki ijayo niwe nimemaliza deni ambalo bado naendelea kuomba ndugu, jamaa na marafiki wanichangie,” alifafanua Senya.

MAJIBU YA CORONA

Alisema wakati mkewe akiwa bado hospitali baada ya kujifungua alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha yuko kwenye timu ya Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye alimjulisha kuwa mkewe ana virusi vya corona.

“Wakaniambia walifanya vipimo kwa bahati mbaya amepata corona.

“Wakaniuliza baadhi ya taarifa ya familia nikwajulisha vyote na baadae wakafika nyumbani wakapuliza dawa na kutuweka karantini kwa siku 14.

“Lakini niliwaambia mimi lazima nitoke niende hospitali wakaniambia nichukue tahadhari zote ikiwemo kuvaa barakoa, kupaka vitakasa mikono pia niepuke kukaribiana na watu hadi sasa katika familia hakuna aliyeumwa kwasababu tunachukua thadhari,”alifafanua.

ASIMULIA ALIVYOJIFUKIZA NA KUPONA

Senya alisema kabla ya mkewe kuumwa yeye ndiye alikuwa wa

kwanza kupata dalili za corona baada ya kwenda hospitalini na baadae kutumia njia za asili alipona .

“Nilianza kuumwa baada ya mteja kufika dukani, nikamwabia mbona una mafua akasema ana mzio, siku 12 baadae nikajisikia vibaya mwili kuchoka nikasema inawezwekana ni malaria.

“Hata baada ya kupimwa na kukutwa na malaria na hata kutumia dawa lakini hali bado haikuwa nzuri, niliporudi tena hospitali niliambiwa nina mchafuko wa damu na malaria wakanipa dawa za nimonia na dawa za vidonda vya tumbo kila nikitumia hali inazidi kuwa mbaya mwili ukawa unawaka moto na mafua kwa mbali sipati harufu .

“Baada ya siku tatu nikaenda hospitali nyingine wakanipima wakasema nina mchafuko wa damu wakanichoma sindano za ‘power safe’ za kwenye mshipa tano lakini kila nikochoma mwili unakakamaa na kukosa pumzi nilikuwa na hofu kwasababu tayari walikuwa wamekwishatangaza wagonjwa wawili wa corona nchini.

“Siku moja nilifanya mazoezi ya kukimbia kutoka Kimanga mpaka External nilivyorudi mwili ukapata nafuu

“Baada ya hapo nikawa na wasiwasi nikaamza kujifukiza na mwarobaini, majani ya mpera, mchaichai, magadi na vitunguu swaumu, maji na tangawizi na mmea unaitiwa ‘Ikingi’ kwa kichaga nilitafuna yale majani siku ya tatu nikaanza kusikia kifua kinaachia mwishowe nikapata nafuu kabisa,”alisema.

DAKTARI WA AGHA KHAN

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana Meneja Mwandamizi, Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Taasisi ya Huduma za Afya wa Aga Khan Tanzania Dk. Olayce Lotha alithibitisha kumpokea mke wa Senya na kumpatia matibabu hadi alipotoka hospitalini .

“Tumempokea huyo mama na hali ya inaendelea vizuri ndio maana tumemruhusu ,tulimpokea tangu tarehe 1 hadi 22 mwezi huu.

“Ninachotaka kuwaambia watu kuwa hospiali ni sehemu salama wasiwe na wasiwasi.

“Hospitali ya Aga Khan ipo kwa ajili ya kusaidia Watanzania hatuna hofu katika kuhudumia, usalama wa wagonjwa ni kipaumbelea namba moja ,utoaji bora wa huduma za afya na kuhakikisha zina ubora.

“Hatutaruhusu Watanzania kufuata matibabu nje ya nchi tunaijenga nchi yetu na kila mtu anapaswa kupata huduma, hatujampokea kwa kuangalia fedha tumemtibu kwanza na kumdai fedha baadae,”alibainisha Loth.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles