32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kuapishwa kwa wateule Chato na Chamwino katikati ya uelewa wetu

Na ABBAS MWALIMU-DAR ES SALAAM 

RAIS Dk. John Magufuli Alhamisi  Mei 21, 2020 aliwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua kushika nafasi mbalimbali za unaibu waziri, ukatibu tawala na mabalozi watakaoenda kumuwakilisha Rais katika nchi walizopangiwa katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Miongoni mwa walioapishwa siku hiyo ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dk. Godwin Mollel Mbunge wa Siha aliyechukua nafasi ya Dk. Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inampa mamlaka Rais kuteua viongozi mbalimbali na kutengua teuzi zao, kama ambavyo inaeleza:

36.-(1)  Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka  ya kuanzisha na kufuta nafasi  za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.      

(2)  Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi unaofanywa na Rais.         

Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2), masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria yoyote inayohusika, mamlaka ya kuwateua watu wengine wote wasiokuwa viongozi wala watendaji wakuu, kushika nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na pia mamlaka ya kuwapandisha vyeo watu hao, kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na mamlaka ya kudhibiti nidhamu ya watu waliokabidhiwa madaraka, yatakuwa mikononi mwa Tume za Utumishi na mamlaka mengineyo yaliyotajwa na kupewa madaraka kuhusu nafasi za madaraka kwa mujibu wa Katiba hii au kwa mujibu wa sheria yoyote inayohusika.      

(4)  Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) hayatahesabiwa kuwa yanamzuia Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu  ya watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Kabla ya kuwaapisha viongozi hawa  Mei3, 2020 Rais Magufuli alimuapisha Dk. Lameck Mwigulu Nchemba kule Chato kuwa Waziri wa Katiba na Sheria baada ya kufariki kwa Balozi Dk. Augustine Mahiga aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo kabla ya kifo chake.

Baadhi ya watanzania walikuwa wakihoji kitendo cha Rais kumuapisha Mwigulu kule Chato huku wengine wakisema alitakiwa kufanyia jambo hili Ikulu ya Dar es Salaam au Chamwino, Dodoma.

Uwanja wa Diplomasia tumeona tutumie nafasi hii kutoa elimu juu ya viongozi kuapishwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kama vile Dar es Salaam, Chato na Dodoma, je katiba inasemaje kuhusu hili?

Tukitazama ibara ya 37 ya Katiba ya Jamhuri ua Muungano wa Tanzania inaeleza kwamba:

37.-(6)   Ifahamike kwamba kiti cha Rais hakitakuwa kiwazi na Rais hatahesabiwa kwamba hayuko katika Jamhuri ya Muungano endapo-

(a)  atakuwa hayupo katika mji ambao ndio makao makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano;

(b)  atakuwa hayupo katika Jamhuri ya Muungano kwa kipindi cha muda wa saa ishirini na nne; au 

(c)  atakuwa ni mgonjwa lakini anatumaini kuwa atapata nafuu baada ya muda si mrefu.

Kwa mujibu wa kifungu (a) cha ibara ya 37 ibara ndogo ya sita ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaona kuwa Rais anaweza kufanya shughuli zake akiwa popote nchini ikiwa ni pamoja na kuapisha na kutengua teuzi.

Ndiyo maana tumeshuhudia mara kadhaa Rais akitengua teuzi za baadhi ya wasaidizi wake akiwa maeneo mbalimbali ya nchi.

Vivyo hivyo kwa mujibu wa Katiba, Rais anaweza kumuapisha kiongozi atakayemteua popote pale nchini.

NI KWA NINI SINTOFAHAMU HII INAJITOKEZA KWA BAADHI YETU?

Nafikiri changamoto hii inatokana na kutofahamu tofauti ya Rais (President) na Taasisi ya Urais (Presidency).

Nitatumia mifano ya Marekani kuelezea tofauti ya Rais na Taasisi ya Urais ili tuweze kuwa na mwanga wa kutosha kwa sababu mfumo wa utawala Tanzania ni muunganiko (hybrid) ya mfumo wa Westminster (Uingereza) na Marekani ambapo unakuwa na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kama viongozi wa juu wa Serikali.

Grossmann (2014) katika kitabu chake ‘New Directions in interest Group Politics’ alitafsiri tofauti ya Rais na Taasisi ya Urais kama ifuatavyo:

“…the presidency-the institution of the president, including the president, White House officials, and all of the associated offices…”

Kwa mantiki hiyo basi kuna Taasisi ya Urais na Rais.

Taasisi ya Urais inajumuisha Rais na watumishi wengine wa taasisi hiyo.

Ndiyo maana hapa kwetu Tanzania tuna Katibu wa Rais, Katibu wa Ikulu, Msemaji wa Ikulu n.k hawa wote ni wafanyakazi wa taasisi hii ya Urais ambayo inaongozwa na Rais.

Taasisi hii ofisi zake ndiyo hizi Ikulu zilizo katika mikoa mbalimbali nchini.

Nae Gelm (2008) alifafanua tofauti hii wakati alipokuwa akizungumzia Ikulu ya Marekani katika kitabu chake ‘How American Politics Works’ aliposema:

“The American Presidency is more than just the president who occupies the White House…the Cabinet, the Executive office of the President, and the White House staff are the three main components of the Presidency. They provide the President the institutional powers to dominate the American political system” (Gelm, 2008:151).

Hivyo basi Ikulu kama taasisi ina uwezo wa kufanya kazi popote katika nchi kama alivyofafanua Dowdle alipoweka mkono wake katika andiko la Eksterowicz na Hastedt (2008:29) aliposema:

“The presidency like most successful institutions, has not been a static creature.”

Dowdle alijaribu kuifananisha taasisi ya Urais na kiumbe na kusema kuwa haiwezi kuwa imeganda sehemu moja tu bali hutembea.

Shida yetu nafikiri inatokana na ufahamu tulio nao juu ya Rais na Taasisi ya Urais kama alivyoeleza Starratt, Robert J (1993) katika kitabu chake ‘The Drama of Leadership’ pale aliposema:

‘But, just as we know almost everything about modern Presidents but far less about the Presidency, as an institution, so we know everything about individual leaders at home and abroad and comparatively little about the complex and wide-reaching process called leadership.’

Kwa maana fupi ya hapa ni kwamba wengi wetu tunamfahamu Dk. Magufuli kama yeye lakini wengi hatuna ufahamu na mchakato mzima wa uongozi na hasa tofauti ya Rais na Taasisi ya Urais ambayo anaiongoza.

Ni imani yangu tumeelimika katika hili la kuapishwa viongozi Dar es Salaam, Chato na Dodoma kwa kutambua tofauti ya Rais na Taasisi ya Urais.

Wenu: Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter) +255 719 258 484 Uwanjwa wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles