29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Corona yageuka vita ya kidiplomasia

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM 

JANGA la virusi vya corona limegeuka na kuwa vita ya kidiplomasia katika pembe mbalimbali duniani.

Unaweza kufikiri Marekani na China tu ambazo zipo kwenye vita hiyo, lakini la hasha! Sweedn, Madagascar na nchi mbalimbali zimejikuta katika migogoro ya kidiplomasia ambayo imebebwa na kivuli cha corona.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani nayo inaonekana kupambana na vita hiyo hiyo.

Hivi karibuni kabla ya mambo kusawaziswa na Rais Magufuli viongozi wa Kenya, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini wanaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki waliamua kufanya mkutano peke yao  pasipo kuishirikisha Tanzania.

Hatua  hiyo ilivuta kumbukumbu ya mkutano kama huo uliowahi kufanyika wakati Rwanda ikiwa na mgogoro na utawala wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete. 

Sintofahamu na maneno mengi kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo wa sasa kabla na baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi kulazimika kufafanua ndani ya Bunge kuwa mkutano huo ulikuwa ni wa Korido ya Kaskazini ilitokana na kumbukumbu hiyo.

Zaidi hatua iliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta ya kufunga mpaka wake na Tanzania kwa kuzuia watu kutoka na kuingia Kenya isipokuwa mizigo nayo ilizusha hali hiyo hiyo.

Kama haitoshi uamuzi uliochukuliwa na Rais Magufuli baadae kumteua Balozi mpya wa Kenya na kumwondoa yule aliyekuwapo Dk. Pindi Chana  na zaidi akimsifu Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu  kwa kuonyesha uzalendo katika mgogoro ulioibuka mpakani hasa baada ya kuzuia watu kuingia na kutoka Kenya nayo ilikuwa na sura hiyo hiyo. 

Hatua ya Rais Cyril Ramaphosa  naye kuitisha mkutano na nchi tano inazopakana nazo (SACU), Botswana, Eswatini, Lesotho na Namibia kujadili juu ya suala la corona huku Jumuiya ya  Maendeleo Kusini mwa nchi za Afrika (SADC)  ambayo Tanzania ndiyo mwenyekiti wake ikiwa kimya, nayo iliibua wasiwasi huo huo. 

Wiki iliyopita wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya wizara yake, Waziri Kabudi alitumia nafasi hiyo  kueleza hali ya diplomasia ya Tanzania hasa baada ya matukio  mpakani mwa Zambia lakini pia serikali kuhusishwa kutohudhuria vikao muhimu vya Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.

Pamoja na Profesa Kabudi kutoa maelezo na ufafanuzi mwingi, jambo lililoacha ukakasi ni kauli yake kwamba mkutano ule uliojumuisha viongozi wa Afrika Mashariki  ulikuwa ni wa Korido ya Kaskazini.

Saa chache baada ya Profesa Kabudi kutoa kauli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dk. Vincent Biruta  alitoa taarifa kuwa mkutano  huo ulikuwa ni wa Afrika Mashariki na kwamba  Burundi na Tanzania ambao wote waliarifiwa hawakushiriki.

Taarifa kwamba mkutano huo wa mashauriano ulifanyika baada ya kukwama kwa mikutano mikuu ya viongozi wa nchi wanachama wa EAC mara ya tatu, nayo ilikuwa sehemu ya mjadala huo.

Kidogo  alichokisema Profesa Kabudi na ambacho kilionekana kufanyika ni kuhusu kilichotokea Zambia ambacho kilileta matumaini ni kuruhusiwa kwa magari  yaliyokuwa yamezuia mpakani.

Hatua hiyo ilileta picha kwamba kulikuwa na mazungumzo nyuma yake  si tu Zambia bali hata Rwanda ambao katika taarifa yao ya kwenye vyombo vya habari iliyotolewa Mei 15 ilieleza hatua zilizochukuliwa za kuondoa vikwazo vilivyokuwa vimewekwa katika mpaka wake wa Rusumo baada ya ujumbe wa Rwanda na Tanzania kufanya mkutano  kwa njia ya ‘video conference’.

Katika taarifa yake Rwanda ilielea hatua walizofikia pande zote mbili za kuondoa  changamoto zilizokuwepo ikiwamo utaratibu wa kubadilisha na madereva mpakani  na kwamba bidhaa zinazoingia Rwanda zitapakuliwa au kupitishwa mahali pa kuingia.

taarifa hiyo ilieleza kuwa utaratibu huo hautahusu malori yanayobeba bidhaa zinazoweza kuharibika na bidhaa za petroli zinazopelekwa Rwanda ambayo yataruhusiwa kufanya kazi kutoka saa 12 asubuhi hadi jioni na yatapelekwa kwa kusindikizwa bila malipo hadi yanakoelekea.

Pia wamekubaliana katika kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, vipimo vitakavyochukuliwa kwa madereva hao wa malori vitakuwa juu ya Serikali ya Tanzania.

Kabla ya taarifa hizi za matumaini kulikuwa na taarifa za madereva wa watanzania ambao walikuwa wamezuia kuingia Kenya, hali kama hiyo ilianzia Uganda na hivyo kuleta mtanzuko.

WAKATI WA KIKWETE

MIAKA  2013 na 2014 ilitawaliwa na mzozo kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda, Paul Kagame. 

Sababu ya uhasama wa marais hao ilikuwa ni hatua ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda kukaa meza moja ya mazungumzo na kundi la waasi la FDLR lililoko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 

Hatua hiyo ilisababisha chokochoko kupitia vyombo vya habari vya Rwanda. 

Japo mara chache Rais Kikwete na Kagame walisikika wakijibizana, lakini  zaidi vyombo vya habari vya Rwanda vilishadidia kwa kuandika habari za kuuponda utawala wa Rais Kikwete. 

Kundi la FDLR linaundwa na Wahutu wenye msimamo mkali waliokimbia nchini Rwanda wakihofia utawala wa Rais Paul Kagame baada ya machafuko ya mwaka 1994. 

Mbali na ushauri huo wa Rais Kikwete, hatua ya Tanzania kupeleka majeshi yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuungana na majeshi ya Umoja wa Mataifa  na yale ya SADC kwa ajili ya kupambana na kundi la M23, nayo haikuifurahisha Rwanda ambayo imekuwa ikitajwa kunufaika na migogoro ya Congo. 

Kundi la M23 linalodaiwa kuundwa na Wanyarwanda wanaoungwa mkono na Serikali ya Rwanda lilipigwa na kufurushwa nchini DRC na majeshi ya Umoja wa Mataifa yakiongozwa na Tanzania mwishoni mwa mwaka 2013. 

Mbali na mzozo huo, mwaka 2014 pia ulishuhudiwa kulegalega kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuungana na kuunda umoja wao uliokuwa ukitambulika kama Coalition of Willing (Umoja wa walio tayari) huku wakizitenga nchi za Tanzania na Burundi. 

Marais wa Kenya, Uganda na Sudan Kusini walikuwa wakikutana bila kuhusisha nchi hizo mbili za Afrika Mashariki kujadili namna ya kuimarisha Jumuiya hiyo katika miundo mbinu, uchumi, biashara pamoja na  kuweka mikakati ya muungano wa kisiasa.

Katika kuonyesha kusikitishwa na muungano huo, Serikali ya Tanzania iliiandikia barua uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kutaka maelezo ya kina kuhusu muungano wa Kenya, Uganda na Rwanda bila ya kuishirikisha katika mipango hiyo ya maendeleo.

Mataifa hayo matatu kwa upande wao yalisema kuwa hayajavunja mkataba wowote wa Jumuiya hiyo na badala yake wanachokifanya ni maendeleo kati yao ambayo yanakubaliwa na Tanzania na Burundi wanaoweza kujiunga nao baadaye.

Mataifa hayo matatu yalikuwa yamefanya mikutano mitatu bila kushirikisha Tanzania na Burundi.

Baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika mikutano hiyo ilikuwa ni pamoja nakujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura; ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudan ya Kusini na kujengwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. 

Kulikuwa pia masuala ya himaya ya ushuru na forodha EAC na pia kuharakishwa kwa shirikisho.

“Sababu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki,” alikaririwa Kikwete akiliambia Bunge Novemba, 2013.

“Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing).

“Hivi ni nani hayuko tayari. Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari.”

Kikwete alisema kwa maoni yake msimamo wa Tanzania kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji ndiyo yaliyokuwa chanzo cha uhasama.

MAREKANI 

Wakati hali ikiwa hivyo kwa upande wa Afrika, Tanzania pia inapambana na changamoto ya kidiplomasia kutoka mataifa  mengine, ikiwamo Marekani.

Marekani ambayo nayo inaongoza kwa wagonjwa wengi wa corona duniani ilitoa taarifa ikitahadharisha raia wake walioko nchini kusalia majumbani.

Taarifa hiyo ilitokana na kile ilichodai kuwa Dar es Salaam imeelemewa na wagonjwa na serikali haikuwa imetoa takwimu zozote tangu Aprili 29 baada ya Rais Magufuli kutilia shaka vipimo vya ugonjwa huo na kuagiza Maabara kuu ya taifa kufumuliwa.

MATAIFA MENGINE

Marekani nchi iliyoendelea na yenye uchumi mkubwa zaidi duniani inayoongoza kwa nguvu za kijeshi, ikichangia asilimia 34 ya matumizi ya kijeshi ya dunia na asilimia 23 ya pato jumla la ndani la dunia nayo ipo katika vita kubwa ya kidiplomasia na China.

Rais wa nchi hiyo, Donald Trump ameashiria kudhoofika zaidi kwa uhusiano kati ya taifa lake na China kuhusiana na mripuko wa virusi vya corona na kudai kwamba  kwa sasa hawezi kuzungumza na Rais Xi Jinping wa China.

Trump amedokeza kwamba anaweza hata kukatisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili. 

Vita ya maneno kati ya Marekani na China ambayo ilianza hata kabla ya virusi vya corona inaonekana kuwa kubwa sasa wakati vifo vilivyotokana na maradhi hayo ulimwenguni kote vimepindukia 300,000. 

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox Business, Trump alisema anasikitishwa na namna China ilivyoshindwa kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 na kwamba janga hilo limeweka wingu katika makubaliano ya biashara ya mwezi Januari na China ambayo hapo awali aliyasifu kuwa ni mafanikio makubwa. 

“Hawakupaswa kuacha hili litokee”, alisema Trump na kuongeza kwamba.

“Jambo baya lilitokea na unaweza kulitazama kama chanzo ni China, lilitokea wakati fulani na lingeweza kuzuiliwa. Tuliwaomba kama tunaweza kwenda na wakasema hapana, hawakutaka msaada wetu. Hivyo nilifikiria nikasema sawa, kwasababu wanajua wanachokifanya. Kwahiyo ilikuwa ama ni ujinga au kutokuwa na uwezo, au ilikuwa makusudi, moja kati ya hizo”, alisema Trump.

MADAGASCAR

Madagascar nayo imo katikati ya vita hiyo ya kidiplomasia iliyosababishwa na janga la corona baada ya Rais wake, Andry Rajoelina kusema kwamba wakosoaji wa dawa ya mitishamba ambayo anaipigia debe kuwa tiba ya Covid-19 inaonyesha tabia ya ubwenyenye ya mataifa ya magharbi dhidi ya Afrika.

Dawa hiyo ambayo Tanzania imeichukua kwa ajili ya kuifanyia utafiti zaidi, Rais wa Madagascar alisema katika mahojiano na shirika la habari la ufaransa 24;  ”Iwapo ingekuwa ni taifa la Ulaya ambalo liligundua dawa hiyo , je kungekuwa na wasiwasi? sidhani”.

Shirika la Afya duniani limeonya dhidi ya kutumia dawa hiyo na Madagascar imekuwa ikijibu mapigo ikisisitiza ilifanyiwa majaribio watu 20 katika kipindi cha wiki tatu.

Muungano wa Afrika pia umesema kwamba inataka kuona data ya kisayansi kuhusu uwezo na usalama wa dawa hiyo kwa jina Covid-Organics.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,609FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles