Amina Omari, Tanga
Hospitali ya Rufaa ya Bombo mkoani Tanga imepokea msaada wa mitungi 50 ya gesi kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wenye tatizo la kupumua.
Msaada huo uliotolewa na kampuni ya oxygen product E .A Company LTD imepokelewa na Mkuu wa mkoa huo, Martin Shigela.
Akikabidhi msaada huo Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Mohamed Abnoor amesema wana lengo la kusaidia wagonjwa wenye uhitaji watakaofikishwa katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga mkuu wa mkoa, Dk. Naima Yusuph amesema hospitali hiyo ilikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo hivyo msaada huo umekuja wakati muafaka.
“Sasa wagonjwa 100 wataweza kupatiwa huduma ya oxygen kwa wakati mmoja kwani mtungi mmoja una uwezo wa kuhudumia wagonjwa wawili, “amesema Dk. Yusuph.