FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imetangaza kuokoa Sh bilioni 11.3 kutoka kwenye vyama vya ushirika (Amcos).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Generali John Mbungo alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ni kutokana na uchunguzi wa awamu ya tatu ulioishia jana Mei 15 mwaka huu ambapo jumla ya Sh bilioni 103.6 zilichunguzwa.
“Kiasi cha fedha zilizookolewa hadi kufikia sasa ni Sh bilioni 11.3, uchunguzi bado unaendelea dhidi ya Sh bilioni 92.3. Ninapenda pia mfahamu kuwa hapo awali Takukuru tulijikita zaidi katika kuhakikisha kuwa fedha za Watanzania waliodhulumiwa haki zao zinarejeshwa.
“Lakini pamoja na jukumu hilo la kurejesha fedha pia tumefanikiwa kuanzisha uchunguzi kwa kufungua majalada ya uchunguzi pamoja na kufungua kesi mahakamani kwa wale ambao hawakutoa ushirikiano katika kufanya marejesho, hii ni kutokana na taarifa mbalimbali zilizopatikana na kubainika wakati tunavyoendelea na zoezi la urejeshaji wa fedha za wakulima katika operesheni hii,”alisema Mbungo.
Aidha katika hatua nyingine kupitia operesheni hiyo, alieleza hali ya uchunguzi na mashitaka ilivyo katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo alisema wamefunga majalada ya uchunguzi 79 katika mikoa mbalimbali nchini.
“Zipo kesi 11 zinazoendelea katika mahakama zetu nchini, yapo majalada 9 ambayo yapo katika mchakato wa kukamilishwa ili tuweze kufikisha watuhumiwa mahakamani.
“Yapo majalada yaliyokamilika na kufungwa baada ya fedha zinazodaiwa kurejeshwa zote au hoja zilizokuwa zikilalamikiwa zimejibiwa zote na pande zote kuridhika, yapo majalada yanayoendelea na uchunguzi kwa kuwa fedha zilizokuwa zikidaiwa zimeanza kurejeshwa lakini uchunguzi umebaini tuhuma za wizi na ubadhirifu, yapo majalada ambayo fedha zilizokuwa zinadaiwa zinaendelea kurejeshwa lakini pia kuna kesi zinazoendelea mahakamani,”alisema Mbungo.