26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatafakari Ebola safari za Hijja

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe

NA ELIZABETH MJATTA

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imesema itafanya vikao na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupata taarifa za sayansi kuhusiana na ugonjwa wa Ebola ikiwa ni hatua ya kuangalia kama safari ya Mahujaji kwenda Hijja itawezekana.

Hatua hiyo ya Serikali imechukuliwa siku tatu baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuutangaza ugonjwa huo kama janga la kimataifa huku safari za Hijja zikitarajiwa kuanza Septemba mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, alisema kwa sasa vikao vinaendelea kwa ajili ya kuweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo.

“Kwa upande wetu sisi tunaangalia zaidi namna ya kuudhibiti kwa hapa ndani. Wenzetu wa Wizara ya Mambo ya nje ndiyo wanahusika na suala la safari, tutaangalia namna ya kukutana nao tuweze kupata taarifa zaidi za sayansi kujua namna gani tunachukua hatua kwa watu wetu,” alisema Dk. Kebwe.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Mahadhi Juma Mahadhi, alisema Serikali inasubiri taarifa za kina kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia kupata usahihi kuhusu ugonjwa huo.

“Hadi sasa hatuna hofu sana lakini kikubwa tutafuatilia taarifa kwa Balozi wetu wa Saudi Arabia tuweze kujua hali ikoje huko,” alisema Mahadhi.

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa masheikh wanaoratibu safari za Hijja nchini kupitia Taasisi ya Tawheed Development Work, Yussuph Machelenga, alisema bado maandalizi yanaendelea ya semina kwa mahujaji wanaotarajia kusafiri kupitia taasisi yao.

“Leo (jana) tumeanza semina kwa mahujaji takribani 100, lakini tunaendelea kusubiri taarifa kutoka Saudi Arabia. Kama wakituzuia kuingia kama walivyowazuia wenzetu wa Nigeria na nchi nyingine zilizopata wagonjwa wa Ebola basi tutavuta subira na tutakwenda kufanya ibada yetu mwakani,” alisema Machelenga.

Ibada ya Hijja kwa Waislamu inatarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu na kuwakutanisha mahujaji zaidi ya milioni tano nchini Saudi Arabia.

Hata hivyo, tayari katika mji ya Jeddah imeripotiwa mgonjwa mmoja mwanamume amefariki dunia kwa Ebola.

Mwanamume huyo anadaiwa kutoka Afrika Magharibi na alikuwa katika hali mbaya tangu alipolazwa huku idara ya afya nchini humo ikiwafanyia uchunguzi wa afya watu waliowasili nchini humo kama njia ya kudhibiti ugonjwa huo.

Tangu kulipuka ugonjwa huo Februari mwaka huu, karibu watu 1,000 wanaripotiwa kufa katika nchi za Afrika Magharibi.

Nchi zilizokumbwa na Ebola ni Guinea, Sierra Leone na Liberia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles