24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Lila awataka waandishi kuzingatia maadili

Jaji Shaaban Lila
Jaji Shaaban Lila

Veronica Romwald na Grace Shitundu, Dar es Salaam

VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuzingatia maadili, weledi na miiko ya uandishi wa habari ili kuepusha migogoro inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Agizo hilo limetolewa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Jaji Shaaban Lila, wakati akizindua Bodi mpya ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Alisema vyombo vya habari vinapaswa kutotumika na vyama vya siasa kwa kuandika habari zenye mrengo mmoja na kuepuka habari za udhalilishaji.

Alisema katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kutokana na baadhi ya vyombo hivyo kuandika habari za udhalilishaji na uchochezi.

“Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi kuwa baadhi yenu (vyombo vya habari), mmekuwa mkipotosha jamii kwa kutoa habari za udhalilishaji na uchochezi, badilikeni hakikisheni mnafuata maadili na miiko ya kazi yenu.

“Kila mtu ana uhuru wa kutoa na kupokea habari kwa mujibu wa Katiba, mmekuwa mkiilalamikia sheria ya magazeti kifungu cha 25 ambacho kinampa waziri mwenye dhamana kutoa adhabu dhidi ya gazeti linalokiuka maadili kwa maoni yake, mnasema kibadilishwe lakini wakati mnasubiri mabadiliko nanyi badilikeni, wekeni maslahi ya Taifa mbele badala ya watu binafsi ili kuepuka migogoro inayoweza kuvuruga amani,” alisema Jaji Lila.

Alisema nchi yoyote yenye demokrasia ni lazima kuwepo na uhuru wa kutoa na kupokea habari unaozingatia mipaka ya upashaji habari.

Aliishauri MCT kuendesha mafunzo maalumu kwa ajili ya waandishi wa habari za mahakamani, ili kuwajengea uwezo wa kuandika kwa umakini bila kuingilia uhuru wa mahakama.

“Kuna mipaka katika kuandika habari za mahakamani kwa mfano ni marufuku kumhoji mshtakiwa nje ya mahakama, lakini imewahi kutokea nchini Kenya katika kesi ya Wangari Maathai, gazeti moja lilimhoji nje ya mahakama na likaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“Ingawaje haijawahi kutokea hapa kwetu lakini ni vizuri tukitoa mafunzo mapema tena muwape na vitambulisho ili tuwatambue, lakini si kama ilivyo sasa ambapo kila mtu anakuja mahakamani akidai yeye ni mwandishi wa habari,” alisema Jaji Lila.

Alisema lazima Bodi ya MCT ibainishe sifa za mtu kuwa mwandishi wa habari ili wafahamike.

Bodi hiyo ya MCT itaongozwa na Jaji mstaafu Thomas Mihayo (Rais) na Makamu wake, Hassan Mittawi huku wajumbe wakiwa ni Rose Haji, Tuma Abdallah, Badra Masoud, Wallace Mauggo, Jaji mstaafu Juston Mlay, Ali Mufuruki na Profesa Bernadetha Killian.

Wajumbe waliomaliza muda wao ni Jaji mstaafu, Dk. Robert Kisanga (Rais), Chande Omar (Makamu) huku wajumbe wakiwa ni Profesa Ruth Meena, Rafii Haji Makame, Kenneth Simbaya na Usu Mallya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles