Mwandishi Wetu -Katavi
KAYA nne za Mtaa wa Rungwa Kata ya Kawajense, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi zimeiomba serikali kuwasaidia fedha na mabati kwa ajili ya kujenga nyumba zao zilizobomolewa na mvua wiki moja iliyopita
Wakizungumza jana waathirika hao walisema kuwa kwa sasa wanaishi kwa jamaa zao wakati wakijipanga kuanza ujenzi upya
Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Agnes Pambe ni mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Rungwa alisema kuwa alikuwa na wadogo zake watatu wakati mvua inanyesha kisha ukuta wa chumba ukaanguka
“Tulikimbilia nje mvua ikiendelea kunyesha na daadae nyumba yote ilianguka,” alisema Agnes
Alisema anaishi na wadogo zake wanne; wawili kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka saba na kuongeza kuwa mama yao anafanya kazi ya kupika mgahawa katika kata ya machimboni na hivyo huja kuwasalimu kila akipata nafasi
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Rungwa, Felicia Mkota alisema alilazimika kuwatafutia watoto mahali pa kuishi kwa msamaria mwema, mpaka mama yao alipokuja baada ya siku tano na kuwapangishia chumba.