Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Ilala, imesema imewaita na kuwapa onyo baadhi ya viongozi wa kisiasa walioanza kutoa misaada mbalimbali ili kushawishi wananchi wawachague katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Christopher Myava, alisema katika uchaguzi wa mwaka huu hawatakifumbia macho chama chochote cha siasa kitakachobainika kinaendesha shughuli za uchaguzi kwa rushwa.
“Tumekwishawaita wale wanasiasa waliokuwa wanajipitisha kutaka kuonekana kuwa wao ndio wagombea katika ngazi mbalimbali na tayari tumewahoji na kuwakanya kuachana na tabia hiyo,” alisema Myava.
Bila kuwataja kwa majina waliohojiwa, Myava alisema wanasiasa wanaotoa msaada wa vitu vya aina mbalimbali ikiwamo fedha wakidai ni msaada, na wao pia watafuatiliwa na taasisi hiyo.
Myava alisema kwa mwaka huu pia wamedhamiria kuwa makini kufuatilia chaguzi za ndani zinazofanywa na vyama vyote nchini.
Alisema chaguzi hizo za ndani ndizo zinakuwa ngumu kwa kuwa zinaambatana na rushwa zaidi.
“Tumejipanga kufuatilia hadi hizo chaguzi za ndani kwa kuwa ndizo zinazoambatana na rushwa kwa kiasi kikubwa na ili ziwe huru na haki, ni muhimu tukadhibiti mianya ya rushwa,” alisema Myava.
Alisema mwanasiasa yeyote atakayegombea katika mkoa huo ajiepushe na utoaji au upokeaji wa rushwa na afuate kanuni za msingi za uchaguzi zilizopo.
Myava alisema ni kawaida yao kutoa elimu juu ya rushwa ya uchaguzi, lakini kutokana na ugonjwa wa Covid-19 hawataweza kukusanya watu kutoa elimu hiyo na badala yake wataitoa kupitia vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Gongo la mboto, Jacob Kisy (Chadema), alisema Takukuru ipo kisheria na inasimamia utendaji kazi wake kwa mujibu wa sheria.
Kisy alisema katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, ni vema taasisi hiyo ikasimamia haki ili kutoa usawa kwa wagombea wote kwakuwa rushwa imekuwa ikipoteza haki.
Alisema katika utekelezaji wa sheria na ufuatiliaji masuala ya uchaguzi, ni vema busara na hekima zikatumika ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa kisiasa.
Kisy alisema kipindi cha uchaguzi ipo michezo michafu ya kuchafuana, hivyo ni muhimu kuwa makini katika utekelezaji wa sheria na kuacha kuwachafua baadhi ya wagombea kwa masilahi ya watu wengine.
“Mazingira ya rushwa huwa yanaonekana, kuna maisha ya kukaa pamoja na kubadilishana mawazo yapo, hivyo katika kipindi cha uchaguzi hakizuii mazingira haya, ila tu endapo yapo kama hayo yanayoashiria rushwa, ni muhimu kumulikwa ili kutoa haki kwa wengine,” alisema Kisy.