29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli awashika pabaya wabunge

RAIS*Azuia safari zao nje ya nchi, watakiwa wawe na vibali

*Baadhi yao wajikuta wakikwama Uwanja wa Ndege VIP

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa Serikali bila kibali, safari hii kibao kimewagekia wabunge baada ya kuzuiwa kusafiri bila ruhusa maalumu, MTANZANIA imebaini.

Hali hiyo imeonekana kuwavuruga wabunge, kwani baadhi yao wamejikuta wakikwama katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, baada ya kubainika kuwa hawana vibali vya kusafiri nje ya nchi.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa, uamuzo huo wa Serikali umegeuka mwiba kwa wabunge ambao wengi wao wamekuwa wakisafiri reja reja kwa kutumia hati zao (Diplomatic  Passport) kwa safari zao binafsi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM), ni miongoni mwa wabunge waliotajwa, ambaye alijikuta akikwama Uwanja wa Ndege katika sehemu ya Watu Mashuhuri (VIP), baada ya kubainika kukosa kibali cha Bunge wala Ikulu kinachomruhusu kusafiri nje ya nchi.

“Huu uwamuzi ni mzuri sana kwani hivi sasa wabunge waliokuwa wamezoe kwenda nje ya nchi kila wakati wanabanwa na katika hili mbunge Martha Mlata ameonja rungu la Serikali.

“… mwishoni mwa wiki iliyopita alikuja hapa Uwanja wa Ndege eneo la VIP na kujikuta akikwama maana kwa sasa eneo la watu mashuhuri kuna orodha ya maofisa na wabunge wote ambao wameruhusiwa kusafiri nje ya nchi kwa vibali aidha cha Ikulu au cha Katibu wa Bunge ambaye kwa sasa hukiomba kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu,” kilisema chanzo hicho.

MTANZANIA ilimpomtafuta mbunge huyo wa viti maalumu ili aeleze kukwama kwa safari yake, alijibu kwa kifupi kwa kusema kwamba hawezi kuchaguliwa pa kwenda.

“Mnanichagulia pa kwenda? Nasema andikieni mnavyojua,” alisema Mlata huku akishindwa kukubali wala kukanusha kuhusu safari yake ilivyokwama.

Masharti ya safari

Kwa mujibu wa masharti yaliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kwa watumishi na viongozi wa Serikali wanaotakiwa kusafiri nje ya nje hutakiwa kuomba kibali kwake.

Baadae kibali hicho huwasilishwa kwa Msajili wa Hazina kabla ya kwenda kwa Katibu ili ajenge hoja ya umuhimu na tija itakayopatikana katika safari husika.

Mbali na hilo pia kwa mtendaji mkuu wa shirika au taasisi wanatakiwa kupima maombi ya safari husika, ili kuona kama yana tija au umuhimu wa kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi, kabla ya kuwasilishwa kwa Msajili wa Hazina.

“Sharti la nne, lina vipengele vitano ambavyo vinatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuwasilisha hoja ya safari ambapo kipengele cha kwanza ni chanzo cha safari husika, cha pili ni faida yake, tatu kwa nini ni muhimu kufanyika safari hiyo na isipofanyika athari yake ni nini.

“Kipengele cha nne kinachambua gharama za safari, kikiweka masharti yanayomtaka mwombaji aainishe gharama ya tiketi ya ndege, posho za safari husika, mlipaji wa gharama za safari na uwezo wa taasisi kifedha.

“Kipengele cha tano cha sharti la nne kinamtaka mwombaji aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na Taifa kama imewahi kufanyika huko nyuma,” yalieleza mashati hayo ya vibali vya safari.

Kauli ya Bunge

Akizungumzia kuhusu vibali vya safari kwa wabunge, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, alikiri kuwapo kwa zuio hilo la safari za wabunge.

Hata hivyo Joel alisema hakuna mbunge aliyezuiwa kusafiri nje ya nchi, kama atafuta taratibu zinazotakiwa iki ni pamoja na kuomba kibali cha Spika wa Bunge.

Alisema pamoja na hali hiyo Bunge halijapokea taarifa yoyote kutoka Ikulu inayozuia wabunge kusafiri nje ya nje.

“Kumekuwa na  taarifa zinazoenea zikisema kwamba rais amefuta safari za nje ya nchi kwa watumishi wa Serikali, si kweli bali alichofanya ni kuwataka wasafiri hawa wa umma kwa kufuata taratibu za nchi,” alisema Joel.

Mkurugenzi huyo alisema wabunge kama watumishi wa Serikali, wanatakiwa kutoa taarifa kwa Spika wa Bunge kabla ya kusafiri nje ya nchi.

“Taratibu kwa upande wa wabunge wanatakiwa kutoka nje ya nchi tangu pale wanapoapishwa kushika wadhifa huo, hivyo kama atakuwa na safari ya nje lazima atoe taarifa kwa Spika.

“…wabunge wanasafiri na Diplomatic Passport inayowatambulisha kama wafanyakazi wa Serikali, hivyo haiwezekani kujiamulia kusafiri bila kutoa taarifa kama taratibu zinavyotaka,” alisema.

Joel alisema utaratibu wa kupewa kibali wabunge wanaosafiri nje ya nchi umekuwapo kwa muda mrefu, lakini umekuwa haupewi uzito.

Rungu kwa waliokaidi

Hivi karibuni Rais Dk. Magufuli, aliowasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa Serikali ambao walikaidi agizo la kutosafiri kwenda nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.

Waliokumbwa na adhabu hiyo kwa kukaidi agizo hilo ni pamoja na watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru).

Waliosimamishwa kazi Takukuru walikuwa ni msemaji wa taasisi hiyo, Doreen Kapwani, Mary Mosha, Ekwabi Mujungu na Rukia Nikitas.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles