27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aliamsha

 MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM

RAIS Dk .John Magufuli amewataka Watanzania kuondoa hofu katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, kwa kuwa ushindi uko mikononi mwetu, baada ya kubaini udhaifu katika vipimo vya ugonjwa huo.

Akizungumza baada ya kumwapoisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba jana, Rais Magufuli alisema wakati Serikali ikiendelea kupambana na maambukizi ya virusi hivyo, tayari wamebaini hitilafu katika mfumo wa upimaji katika Maabara Kuu ya Taifa, hivyo hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa kwa ajili ya kuwa na uhakika wa matokeo ya vipimo vya corona katika maabara hiyo.

“Pale National Referal Laboratory inayohusika kupima corona kuna controvecial (utata) nyingi za ajabu hasa baada ya kufuatilia na kutaka kujua uhakika wa vipimo.

“Katika kufuatilia uhakika wa vipimo, Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Prof. Mabele Mchembe alikwenda na kuchukua sampuli za mbuzi, kondoo, papai, oil ya gari na vitu vingine na kupelaka maabara bila wahusika kujua.

“Sampuli ya oil ilipewa jina la Jabir Hamza (30) ilileta majibu negative (haina maambukizi), sampuli ya fenesi iliyopewa jina la Sarah Samwel (45) matokeo yalikuwa unconclusive (haikuonesha majibu), sampuli ya papai iliyopewa jina la Elizabeth Anne (26) ilileta majibu positive (imeambukizwa).

“Pia sampuli ya ndege kware positive(imeambukizwa), sungura undeterminant (haikubainika), mbuzi akawa positive(imeambukizwa), kondoo akawa negative (haijaambukizwa). Sasa tukishaona umepeleka sampuli ukamwambia huyu ni binadamu ikawa positive (imeambukizwa) basi ile jamii yote inatakiwa kuwekwa isolation, kwa hiyo yake mapapai, kware, mbuzi wote walitakiwa watengwe,” alisema.

Alisema anatoa nafasi pia kwa wanasayansi wengine kufanya uchunguzi huo kwa kuchukua sampuli mbalimbali na watakuja kubaini kwamba kile anachokizungumza kina ukweli.

“Kwa hiyo narudia kuwaeleza Watanzania, bado tuko kwenye elementary stage (hatua za awali), tusitaharuki na watu waendelee kuchapa kazi, tusitishane, na wanasiasa waache kuitumia hii kama agenda kwa sababu haitawasaidia,” alisema. 

Rais Magufuli alieleza kuwa uzoefu unaonesha ni kawaida kuwa kila gonjwa jipya linapotokea watu hupata wasiwasi kama ilivyotokea kwa ugonjwa wa Ukimwi lakini leo hata watu wanaobainika kuambukizwa Virusi vya Ukimwi wanakwenda kuposa na kuoa.

Alisema wakati wa ugonjwa wa surua ilikuwa marufuku hata kwenda kutembelea eneo hilo na imekuwa hivyo hivyo kwa magonjwa kama ukoma na Kifua Kikuu (TB), ebola, zika, hofu zimekuwa zikijengeka lakini matatizo hayo hatimaye yalipatiwa ufumbuzi.

“Unakuta mtu anazungumza funga Dar es Salaam, funga Tanga, sifungi, nilishasema. Ni lazima Watanzania tuishi tuchape kazi na tuendelee kuchukua tahadhari na kwa kweli siku zinazokuja ninafikiria hata kuruhusu ligi ziendelee ili watu wawe wanacheza na watu wawe wanaangalia kwenye TV, tuweke utaratibu mzuri kwa sababu ninaelewa hata kwa walioathiriwa sana na corona sijaona mwanamichezo yeyote ambaye amedhurika sana.

“Na hii inadhihirisha wazi kwamba kwa wale wanaofanya mazoezi corona inawakwepa, sasa kama tunawazuia hata kucheza mpira, maana yake tunawaambia waugue corona. Kwa hiyo itafika mahali ninajaribu kuendelea kusubiri wataalamu wangu wanishauri vizuri kwamba hata ligi ikiwezekana tuendelee kucheza. 

“Inawezekana tunaweza kuendelea kuishi na huu ugonjwa kama wanavyoishi watu wenye Ukimwi, TB, Surua na maisha yakaendelea, tuache kuogopana na kutishana.

“Inawezekana hilo fenesi ingekuwa na lenyewe linasikiaga labda na lenyewe lingekuwa limeshaoza kwamba lina corona. Inawezekana lile papai lingeambiwa lina corona ingewezekana sasa lingekuwa limeshaoza kabisa. Lakini kwa sababu lenyewe halisikii lina corona na lipo,” alisisitiza.

Alimwagiza Waziri Dk. Mwigulu Nchemba, akashirikiane na Wizara ya Afya wakaangalie upya kwenye hiyo maabara kuu kuna nini ndani na kama kuna kitu kama jinai ishugulikiwe kisheria na kama kuna watu walijihusisha kwenye jinai kwa kutumia hivyo vifaa basi sheria ichukue mkondo wake, lakini pia kama vifaa vina matatizo ya kiufundi lazima pia viangaliwe.

“Nilishasema tusikubali kila msaada tukafikiri ni kwa faida ya nchi hii. Mnaweza mkaambiwa kuwa wote mna corona na ndiyo maana utakuta wengi walioambiwa kuwa wana corona mpaka sasa bado ni wazima,” alisema.

Mkuu huyo wa nchi, aliwataka watanzania wasimame imara hili lisiwayumbishe na anajua kuwa wapo ambao wangependa sana kuzungumza juu ya corona na kuna vyombo vingine vya habari muda wote vinazungumzia corona muda wote, akisisitiza kuwa hii ni vita ya aina nyingine

Alisema corona kweli ipo lakini isiyumbishe Watanzania katika msimamo na mwelekeo, wasitishwe na aliendelea kutoa wito hasa kwa vijana ambao muda mwingi wanapost watu wakisema wamekufa kwa corona. 

DAWA MADAGASCAR

Rais Magufuli alisema anaendelea kuwasiliana na Madagascar na tayari wameshaandika barua wanasema kuna dawa zimepatikana kule, hivyo atatuma ndege kule na dawa hizo zitaletwa nchini ili Watanzania pia waweze kufaidika nazo. 

“Kwa hiyo Serikali imekuwa inafanya kazi usiku na mchana na kwamba hata kama niko Chato, huu ndiyo wakati ambao watu wanatakiwa kusimama pamoja,” alisema.

JAJI MKUUMSTAAFU

Rais Magufuli alisema walihangaika sana na afya ya Jaji Mkuu mstaafu alkiyefariki dunia mwanzoni mwa wiki, Augustino Ramadhani kwa karibu mwaka mzima japokuwa si vyema kutaja matatizo yake, lakini walimpeleka India na mara ya mwisho walichukua ndege na kumpeleka Nairobi, na kwamba amefariki kwa saratani ila watu wamebadilisha maneno ya ajabu.

Alisema si vyema kudai kwamba kila mtu anayekufa anakufa kwa corona kwa kuwa magonjwa mengine kama malaria, ajali pia zinaua watu wengi hivyo Watanzania ni vyema wabadilike waache kuchafua nchi kwa sababu suala hili Mungu atalisimamia na tutavuka salama.

Alimpongeza Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Afya, Prof. Mchembe kwa hilo la kufanyia vipimo sampuli za mapapai na mafenesi kwa kuwa katika hilo wamekwenda na mabadiliko na kumtaka aendlee hivyo hivyo pamoja na watendaji wake walioko katika wizara ya afya.

Aliema kuna mambo mengi ya kushangaza yanafanyika katika nchi hii akimtaja Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye siku moja alizungumza akisema kuwa Mkuu wa Wilaya hawezi kusafirishwa kwenda kwao na kuzikwa mkoani humo, na kwamba hiyo inasikitisha sana, kwa kuwa haiingii akilini akihoji kama madaktari wanakwenda kuwaona wagonjwa wakiwa wamevaa hizo PPE wakiwa wamezuia na corona, viongozi wa Mkoa wa Mtwara walishindwaje kuufunga mwili wa marehemu PPE na kuusafirisha kwenda Moshi kwa heshima zake?

“Niwaombe viongozi wenzangu tusichukulie hili kwa papara, tutumie wataalamu kupata reasons zitakazotusaidia kuwahudumia hata kama wapo watakaopata matatizo kutokana na ugonjwa huu wa corona. 

“Ninaamini corona ipo lakini siyo kwenye extent hiyo. Kwa taarifa nilizokuwa ninazijua katika siku mbili tatu zilizopita ni kwamba watu waliofariki kwa corona ni 16, sasa unaweza kucompare tu ratio (uwiano) ya 16 kwa idadi ya watu milioni 60, piga na uwiano wa sehemu nyingine ukilinganisha na idadi ya watu wao utaweza kuangalia ni nchi gani ambayo watu wake wamekufa wengi,” alisema.

Alisema lakini watu wanawaogopesha Watanzania wengine wanaogopa hata kwenda kufanya kazi wengine wanaogopa kwenda sokoni, lakini pia nchi zilizofunga miji matokeo yake wako wazi, kwa kuwa kuna nchi ambazo watu zaidi ya 50,000 wamekufa na zina uwezo wa kila kitu.

“Kwa hiyo mambo ya kucopy na kupest hatuwezi kuyafanya katika nchi hii hivyo ninawaomba watanzania waendelee kuchapa kazi na kuchukua htahadhari pia wawapuuze wanaojaribu kuwatisha huku wakiendela kumuomba Mungu,” alisema. 

VIONGOZI WA DINI

Rais Magufuli alisema wapo hata viongozi wa dini wameanza kuyumba na kumsahau Mungu na wameanza kuweka ubinadamu mbele, wakiwataka watu waache kuomba na wajiokoe, lakini katika kipindi hiki cha mpito mengi yatasikiwa na huu ndio wakati wa kupima viongozi waliopo.

Aliwataka viongozi wa dini kuwa huu ndio wakati mzuri wa kutangaza wale walionuia kuyahubiri kwa kuwa wapo mashahidi waliosimama imara katika kipindi kigumu na wajitoe kutumia ahadi zao kuwaimarisha watanzania katika tatizo hili la ugonjwa.

Aliwataka Watanzania waendelee kumuomba Mungu na atawapitisha katika changamoto hii na kwamba Serikali iko vizuri na biashara zinaendelea ndiyo maana wanaweza hata kulipa mishahara 

Alisema katika miezi mitatu iliyopita Serikali imeendelea kulipa walimu japokuwa hawafundishi na wataendelea kwalipa pamoja na watumishi wengine, suala ambalo nchi nyingine zimeshindwa.

KUHUSU MBATIA

Rais Magufuli alisema alimpongeza Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kuwa mwanasiasa mzuri kwa kuwa amekuwa akimuunga mkono na kwamba amekuwa hata akimwandikia ujumbe mfupi wa maneno ‘Uwe na moyo Mkuu, tuendelee kuchapa kazi’ akisema kwamba ni mwanasiasa wa upinzania lakini angalau ni mwelewa kwa kuwa unaona kabisa kuwa anaangalia masilahi ya Tanzania.

POSHO KWA WABUNGE

Mkuu huyo wa nchi, alisema kuwa utakuta mtu mwingine anazungumzia Dar es Salaam kuwa wanaahirisha kwenda bungeni wakati wala hayuko bungeni, akiwataka waache na kwamba tayari ameshatoa maagizo wasilipwe posho ambayo hawaifanyii kazi bali watalipwa na hao mabeberu wanaowatuma kuzungumza hayo wanayoyazungumza 

 Alisema Watanzania wasikumbali kutumika kwa kuwa corona haiko Tanzania tu bali iko katika nchi karibu zote duniani hivyo wasiitumie hii kama base kwa sababu kwanza huu ugonjwa wala haukuanzia hapa.

Alisema wale wanaoendelea kufanya mbinu za kijinga kama hizo kwamba papai, kware, mbuzi vina corona ni lazima katika mtazamo wa kisayansi watu wafanye kazi, hivyo wataalamu wetu katika vyuo vikuu vyote huu ndio wakati wa kufanya kazi na kuonyesha uwezo wao wa kufanya tafiti kwa sasa.

Alisema hana uhakika na mkuu wa maabara hiyo kwa kuwa hatab yeye hakujulishwa wakati wanapeleka sampuli hizo lakini hata yeye alitakiwa kufanya uhakiki wa utendaji wa mashine zake katika siku za nyuma 

PONGEZI KWA MWIGULU

Alimpongeza Dk. Nchemba kwa kumwapisha mara ya pili na kumtaka akafanye kazi na amtangulize Mungu, akiangalia jukumu lake la msingi ambalo ni kuhakikisha Wizara ya Katiba na Sheria kama ilivyoongozwa vizuri na mtangulizi wake, Balozi Dk. Augustine Mahiga aliyefariki Ijumaa iliyopita akasimamie na kutekeleza yale yote aliyofanya kwa kuwa alifanya kazi yake vizuri sana.

Alisema vijana wengi hawajamwangusha hivyo ni vyema akasimamie hilo kwa maslahi ya nchi huku akiwataka Watanzania kutokubali kuwekwa hofu kwa kuwa ni kitu kibaya sana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles