27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JANGA LA CORONA Utabiri wa Benki ya Dunia na hali halisi ya maisha Dar es Salaam

Na MWANDISHI WETU

ULE utabiri wa Benki ya Dunia kwamba  uchumi wa Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara utaporomoka kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu miaka 25 iliyopita,kutokana na virusi vya Corona, ni kama unaakisi hali ya sasa hususani kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambalo kwa sasa ndilo linaloongoza kwa Visa vingi vya maambukizi ya ugonjwa huo ukilinganisha na mikoa mingine nchini Tanzania.

Japo Serikali imetangaza kutofunga shughuli zozote zaidi ikiwatahadharisha wananchi wake kuchukua tahadhari katika maeneo yenye mikusanyiko, lakini shughuli za wengi ni kama zipo nusunusu.

Kwa majibu wa sensa ya mwaka 2012, ambayo ilitoa mwanga juu ya idadi ya Watanzania waliopo kwenye shughuli rasmi ambao idadi yao haipiti asilimia 30 na wao kutegemewa na asilimia 70 iliyobaki, wengi wao sasa wanalia hali ngumu.

Baadhi ya waliokuwa wanajishughulisha na shughuli ndogo ndogo kama biashara na nyinginezo sasa wanakwambia si tu nauli ya kuwawezesha kufika katika shughuli zao bali hata  mlo wa siku moja ni mbinde.

Vijana wadogo waliofika katika jiji la Dar es Salaam  ambalo hukusanya mamilioni ya watu wanaotoka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutafuta maisha wanakwambia hata zile biashara  zao wanazouza kwa kutembeza barabarani zimekuwa mbinde kutoka.

Hali kama hiyo inafanana na wale wenye maduka makubwa ambao baadhi yao sasa wameyafunga na wale wanaoendelea kufanya biashara hizo wanasema mapato yao yameporomoka tangu maambukizi ya virusi vya corona yatangazwe kufika nchini Machi 16 mwaka huu.

“Hali ikiendelea hivi, sijui huko mbele itakuwaje? Nawaza sipati jibu, Kwani nina familia inahitaji kula….bahati nzuri shule zimefungwa kuna gharama kidogo zimepungua lakini kiukweli hali mbaya nawaza nitafanyaje”.

“Naogopa corona, lakini nikiwaza nitaimudu vipi familia yangu, naona corona ni afadhali tena kuliko ninachokiona mbele,” anasema Ibrahim Haji ambaye ni mmiliki wa duka la vifaa vya magari katikati ya jiji la Dar es Salaam.

MTANZANIA Jumapili limefika mara kadhaa katika eneo la Kariakoo hadi Lumumba karibu kabisa na ziliko ofisi za chama utawala cha Mapinduzi (CCM), na kushuhudia Jumatatu kama Jumapili yaani pilika pilika za eneo hilo ambalo lina madalali wengi na wale wanaoendesha shughuli za kutengeneza magari na kuuza vifaa vya magari zikiwa zimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Unayaona maduka haya?”.fundi mmoja wa magari katika eneo hilo anamwonyesha mwandishi wetu na kuongeza;

” Kwa sasa baadhi yamefungwa, hakuna fedha, ‘movement’ za watu huku zimepungua kabisa kila siku huku ni kama Jumapili kwa sasa”.

“Wapo ambao wamefunga kwa sababu huenda wanaogopa corona, lakini wengine hali mbaya, huku watu ni wachache sasa labda kule mtaa wa Kongo au sokoni kuna watu lakini sio huku, ” anasema fundi huyo magari.

” Kuna jamaa yangu aliajiriwa katika duka moja huku la kusambaza vyakula ambalo makao yake makuu yapo Arusha kwa sasa wamefunga shughuli” anasema.

Gloria Swai ambaye anamiliki duka la maji ya kunywa katika eneo la Kijichi naye anaweza kuwa na ushuhuda mzuri wa hali ya sasa na utabiri wa benki ya dunia.

Anasema kwa mwezi alikuwa anakusanya milioni moja lakini kwa sasa hata kufikia mauzo ya shilingi laki tatu ni mtihani.

” kuna mambo mengi labda wakati mwingine nasema ni kwa sababu ya hali ya hewa kwa sababu biashara yangu inategemea jua, watu wakaukiwe wanywe maji, wakati mwingine nasema hapana mbona mwaka jana nyakati kama hizi nikiangalia kwenye daftari la mauzo nilikuwa nafanya vizuri?”.

” Kwa hiyo pia unaweza kuona athari za corona, hapa nahitaji kulipa kodi ya TRA, leseni ya Manispaa ambalo pia wametuongezea fedha nyingine wanasema sijui levy duty mbali na ile ya leseni, ‘trend’ ikiwa hivi naona nitafunga tu biashara kwa sasa sioni faida zaidi ya hasara na ukumbuke kodi ya mwenye fremu iko palepale  na kodi nyingine za serikali  sasa namfanyia kazi mwenye fremu?” Anasema.

Simulizi za wafanyabiashara hawa wadogo hazitofautiani na za wale wakubwa wote wanalia hali mbaya zaidi wanafiria kodi.

Lusajo John ambaye anafanya biashara ya mafuta katikati ya jiji la Dar es Salaam anasema mauzo yake yameporomoka kwa zaidi ya asilimia 90.

Anasema kwa siku alikuwa ana uwezo wa kuuza lita 750,000 hadi 800,000 lakini kwa sasa anaishia kuuza lita 20,000 kwa siku.

Anasema mafuta mengi aliyokuwa akiuza ni yale ya ndege ambayo kwa sasa ni kama hauzi tena.

Safari nyingi za ndege za kimataifa ni kama nazo hazipo tena nchini Tanzania baada ya mashirika makubwa ya kimataifa kusitisha ili kupunguza kazi ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona hali kadhalika na nchi nyingi duniani ni kama bado zimefunga mipaka.

Hali kama hiyo ndiyo inayowakumba wakulima wakubwa.

Mmoja wa wakulima wakubwa ambaye alizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotaka jina lake litajwe anasema kama hajapata ‘stroke’ au shinikizo la damu wakati huu basi tena.

Anasema yeye ni mkulima mkubwa wa parachichi na amekuwa akiuza nje ya nchi lakini baada ya nchi kufunga mipaka kwa sababu ya corona maparachichi yake yameishia kuoza ndani ya kontena.

Anasema kibaya zaidi kilimo chake amekuwa akikiendesha kwa mkopo kutoka benki.

“Najiuliza nitalipaje, kwa kweli hali ni ngumu mno, kama huko nimechemka najiuliza nini nifanye nilipe mkono, hakuna!”.

Pengine kwa kutambua hali mbaya ya uchumi baadhi ya nchi hususani zile zenye uwezo mkubwa duniani zimechukua hatua ya kunusuru wananchi wake, nchi maskini jambo hilo limekuwa mtihani kwake.

Marekani taifa kubwa duniani kiuchumi, limechukua hatua kadhaa ikiwamo kutenga dola trilioni 12 na hivi karibuni tena dola nusu bilioni kwa ajili ya raia wake waliopoteza ajira kwa sababu ya janga la corona.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni Benki ya dunia ilisema mripuko wa virusi vya Corona unaozidi kusambaa unatarajiwa kuzisukuma nchi za Afrika,Kusini mwa Jangwa la sahara katika mporomoko wa kiuchumi katika mwaka huu 2020 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25. 

Ripoti ya benki ya dunia kuhusu hali ya kiuchumi barani Afrika imesema kwamba uchumi wa bara hilo utashuka asilimia 2.1 na kufikia asilimia 5.1 kutoka kiwango cha ukuaji cha mwaka jana cha asilimia 2.4.

Aidha mripuko huu wa virusi vya Corona utazigharimu nchi za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika dola bilioni 37 hadi dolla bilioni 79 ambayo ni hasara itakayoonekana mwaka huu kufuatia kuvurugwa kwa shughuli nyingi za kibiashara na kiuchumi miongoni mwa sababu nyinginezo.

Makamu mwenyekiti wa benki ya dunia kwa ajili ya Afrika, Hafez Ghanem amesema janga la ugonjwa wa Covid-19 linapima uwezo wa mwisho wa jamii na nchi zote ulimwenguni na kuna uwezekano hususan kwa nchi za Afrika kuathirika zaidi.

Benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF zinakwenda mbio kutoa fedha za dharura kwa nchi za Afrika na nyinginezo kukabiliana na virusi vya Corona ili kupunguza athari zitakazosababishwa na hatua za kufungwa kwa shughuli za kimaisha zinazochukuliwa nchi mbali mbali ulimwenguni kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo vya Corona.

Ikumbukwe kwamba janga la virusi vya Corona limesababisha kufutwa kwa safari za kimataifa katika nchi nyingi za bara hilo la Afrika hali ambayo imeathiri kwa kiwango kikubwa sana sekta mbali mbali kama vile sekta ya utalii.

Serikali mbali mbali za bara hilo la Afrika zimetangaza hatua ya kufunga miji au nchi kwa maana ya kwamba hakuna shughuli za kawaida za kimaisha haziruhusiwi tena kufanyika au baadhi ya nchi zimetangaza kuzuia watu kutoka nje,hizi zikiwa ni hatua zinazodhamiriwa kupunguza kusambaa kwa virusi vya Corona ambavyo kwa hakika vimechelewa kuingia Afrika lakini sasa vinasambaa kwa kasi kubwa barani humo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kutokana na hali hii benki ya dunia inasema  ukuaji wa pato la ndani utapungua kwa kiwango kikubwa na hasa katika nchi tatu zenye uchumi mkubwa katika bara hilo,Nigeria,Angola na Afrika Kusini. 

Kadhalika nchi zinazouza mafuta pia zitaathirika sana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles