28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kanisa Katoliki Tabora kutoa vifaa vya kujikinga na corona

NA ALLAN VICENT, Tabora

TAASISI ya Maendeleo ya Jamii iliyoko chini ya kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora (CARITAS), inatarajia kutoa vifaa vyenye thamani ya Sh mil 4.2 kwa wakazi wa vijijini mkoani hapa ili kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. 

 Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Timothy Chombo, alipokuwa akihitimisha mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo watumishi wake.

Alisema Kanisa Katoliki kupitia taasisi hiyo limeendelea kutoa misaada miongoni mwa jamii ili hakikisha watu wenye uihitaji wanaishi maishi bora na sasa wameamua kusaidia juhudi za Serikali katika kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

 Alisema wanatarajia kutoa  ndoo 30 zenye thamani ya Sh. 720,000, lita 100 za vitakasa mikono zenye thamani ya Sh 1,800,000, lita 100 za sabuni ya maji zenye thamani ya Sh 980,000 na barakoa 720 zenye thamani ya Sh 720,000.

alisema vifaa hivyo vitakabidhiwa katika vijiji vya kata za Ndevelwa, Ifucha, Tumbi na Itetemia kwa wakulima na wafugaji waliopo kwenye mradi unaoendeshwa na taasisi hiyo katika maeneo hayo.

Chombo alisema mafunzo waliyowapa watumishi hao yalilenga kuwapa elimu ya namna ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona ili waweze kwenda kutoa elimu hiyo kwa jamii ili ijue namna ya kujilinda na janga la ugonjwa huo.

alisema jamii imeonekana kukata tamaa na kuwa na hofu kubwa juu ya ugonjwa huo hivyo elimu hiyo itawaondolea hofu na kuwapa elimu sahihi ya kupambana na maambukizi hayo na kurejesha amani miongoni mwao.

Alisema kupitia mafunzo hayo wataelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya barakoa za kushonwa zenye vitambaa vitatu zilizopendekezwa na Serikali ambazo zinaweza kufuliwa na kunyooshwa kwa pasi na kutumika kwa muda mrefu.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Augustino (SAUT) tawi la Mwanza, Padri Leons Maziku ambaye pia ni mtaalamu wa mambo ya saikolojia, alisema mafunzo hayo yatawapa mwanga, mwongozo na maelekezo sahihi ili kutambua mbinu za kujikinga na ugonjwa huo.

Alisema mafunzo hayo yatawasaidia kutambua tatizo, kujilinda, kuwalinda na kuwaheshimu waathirika wa janga hilo pamoja na wasioathirika na kutowabagua kijinsia, umri, dini, dhehebu, kabila, elimu na kuwa wavumilivu na wasikivu zaidi wakati wa kuwapatia elimu hiyo.

Alisema kuwa kupitia maombi ya dhati kwa Mungu, elimu ya sayansi na saikolojia ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kama vikizingatiwa vizuri zaidi mapambano dhidi ya janga hilo yatafanikiwa na hatimaye kulimaliza kabisa janga hilo hatari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles