27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI RAMADHANI, BALOZI MAHIGA Miamba iliyozaliwa mwaka mmoja yazikwa siku moja

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MWANADIPLOMASIA Nguli, Balozi Dk. Augustine Mahiga na Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, wamezikwa leo huku viongozi mbalimbali wakisema taifa limepoteza watu waliokuwa na weledi na unyenyekevu.   

Balozi Mahiga ambaye alifariki dunia juzi alizikwa kijijini kwao Tosamaganga mkoani Iringa wakati Jaji Ramadhani aliyefariki dunia Aprili 28, alizikwa katika makaburi yaliyopo Kimara King’ongo Dar es Salaam.

Viongozi hao waliopishana siku tatu kufariki duania na wote kuzikwa jana, walizaliwa mwaka 1945, ambapo Mahiga alizaliwa Agasti na Ramadhani Desemba.

Samia aongoza maziko ya Balozi Mahiga

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye alimwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika mazishi ya Balozi Mahiga, alisema marehemu wakati wa uhai wake aliwakilisha vyema nchi kutokana na umahiri wake wa masuala ya diplomasia na hivyo kuitangaza vyema kimataifa.

“Serikali imempoteza mtu ambaye alikuwa na mchango mkubwa na uzalendo wa hali ya juu, wakati akiwa mjumbe wa baraza la mawaziri mara zote amekuwa mshauri mzuri katika kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na jumuiya za kimataifa na hakupenda kuonekana kama yeye ni mjuzi na ana upeo wote huo wa uzoefu,” alisema Samia.

SALAMU ZA BUNGE

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema Bunge limepoteza mtu ambaye alikuwa akiwasaidia na hata bajeti yake ni kati ya bajeti zilizopita kirahisi kwa sababu ya weledi wake.

 “Tulimfahamu kama mtu mwenye weledi wa hali ya juu sana, mtu mwenye ufahamu wa hali ya juu, mtu mwenye akili nyingi, mtu mnyenyekevu, mtu mwenye upendo.

“Kipindi cha bajeti mnafahamu ni kipindi kigumu kwa upande wa mawaziri, lakini waziri huyu kila mbunge alimpenda na bajeti yake ni kati ya bajeti zilizopita kirahisi sana kwa sababu ya weledi wake kwa namna ya kueleza hoja zake, namna anavyozileta mbele ya Bunge.

“Kwa hiyo na sisi tumempoteza mtu ambaye tungetamani kumuona lakini yako yale ambayo tumejifunza kwake nasi tutaendelea kupita katika hayo.

“Ndugu yetu ametangulia na tumeelezwa tabia zake njema je, sisi wakati wetu utakapofika watu wanalo la kujifunza kutoka kwetu? Hilo ni swali ambalo kila mmoja wetu lazima ajiulize 

“Tunaweza kusema ndugu yetu alipata ama alizitafuta fursa nyingi, akaenda duniani kote, salamu zake zinatoka kila mahali, lakini sisi tutoe mchango katika lile eneo tulilopo kwa sababu si kila mmoja atapata fursa kama hizi alizozipata ndugu yetu,” alisema Dk. Tulia.

Katika Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, alisema Balozi Mahiga alipenda kusikiliza wadogo na hata kama hafahamu anachoelezwa alikuwa akisikiliza ili kupata kufahamu zaidi.

“Hakika ni nadra sana kupata kiongozi wa aina hii, tutaendelea kumuenzi, alikuwa ni mtu wa watu, alipenda watu, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuongea na kila mtu aliyekutana naye.

“Hakika ameacha simanzi kubwa katika familia yake, taifa letu, wafanyakazi katika Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje, mabalozi, wana Iringa na marafiki zake wengi waliopo hapa nchini na hata duniani kwa ujumla,” alisema Profesa Mchome.

Akitoa salamu za Mahakama, Jaji Mfawidhiwa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Panterine Kente, alisema Balozi Mahiga afariki kishujaa kwani amefanya mambo makubwa ambayo viongozi wengine wanastahili kuyaiga.

USALAMA WA TAIFA

Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Diwani Athumani, alisema Balozi Mahiga alijiunga na idara hiyo mwaka 1976 na alitekeleza majukumu yake vizuri katika nafasi mbalimbali.

“Tuna mambo mengi sana ya kukumbuka na kujifunza, alitimiza utumishi wake ndani ya idara lakini aliendelea kuonyesha uzalendo wake ndani ya nchi yake.

“Siku nne kabla ya mauti niliongea naye sauti yake ikionekana ina nguvu, mtu mwenye afya na tulikubaliana mambo kadhaa lakini kabla hatujayafikia mauti imemfika, hakika kwa idara tutamkumbuka” alisema Athumani.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, alisema wana Iringa wamepata pigo kwa kumpoteza kiongozi ambaye alikuwa akijinyenyekeza kwa jamii.

“Dk. Mahiga ameondoka lakini kitabu cha maisha yake bado kinaendelea kuishi, sisi kama vijana viongozi tumejifunza kwamba unyenyekevu ni jambo muhimu katika uongozi, kujishusha kwake usikivu wake, upendo wake, kutokuwa mtu mwenye mabega na kujionyesha ni somo kubwa tumebaki nalo katika maisha yetu na katika utumishi wetu,” alisema Hapi.

Balozi Dk. Mahiga ameacha mjane, watoto na wajukuu kadhaa.

JAJI RAMADHANI ALIJITABIRIA KIFO

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sothenes, alisema Jaji Ramadhani ameacha alama ambayo haitafutika kwa kanisa na kwamba maisha yake ya ucha Mungu, uadilifu, unyenyekevu, upendo, ukarimu na amani yataendelea kuwa fundisho kwao.

“Nakumbuka siku moja miaka mitatu iliyopita nikiwa naongoza ibada yeye akiwa ni muhubiri na wakati huo alikuwa ametoka kwenye matibabu nchini India, mwili wake ulionekana umechoka, yuko dhaifu na wazo kuu la siku ile katika mahubiri lilikuwa linasema kumtegemea Mungu.

“Alipokuwa akifundisha akasema tunapozungumza kuhusu kumetegemea Mungu haijalishi unapita katika changamoto ngumu kiasi gani, na akajitolea mfano yeye mwenyewe, akasema nipo katika hali ngumu, maumivu makali lakini bado imani yangu inanisogeza kumtegemea Mungu.

“Akasema nilimuomba Mungu aniponye lakini uponyaji wa Mungu una maeneo mawili makubwa, ama Mungu aondoe maradhi katika mwili huu nibaki kuwa salama, huo utakuwa ni uponyaji.

“Au ikimpendeza hata achukue roho yangu aitoe katika mwili huu wa maradhi pia itakuwa ni uponyaji, akasema hayo yote yanadhihirishwa kumtegemea Mungu katika maisha yetu…maneno yale yaliwatia nguvu wengi na wengine hata kutoa machozi,” alisema Askaofu Sothenes. 

Naye Askofu Nelson Kisare kutoka Kanisa la Menonite Tanzania alisema; “Mwaka juzi nilikuwa na baba yetu katika kongamano la maombi ya maziwa makuu linalofanyika kila mwaka kule Kampala Uganda, niliuona mchango wake, tunamuona jinsi alivyokuwa ameshika imani.

Jaji Ramadhani alifariki dunia Aprili 28 asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan, Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Taarifa zilizotolewa na Mahakama ya Tanzania zilieleza kuwa Jaji Ramadhani alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani.

Aidha Balozi Mahiga ambaye alikuwa akihudhuria vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea, aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma alfajiri ya Mei Mosi na alifikishwa hospitali akiwa ameshafariki. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles