29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kanisa latoa nguo kwa wenye ukoma

NA ALLAN VICENT, Tabora

 KANISA la Free Pentecoste (FPTC) Kituo cha Ipilili wilayani Nzega mkoani Tabora, limetoa msaada wa mavazi yenye thamani ya Sh 650,000 kwa wakoma wanaolelewa katika Kijiji cha Iduguta wilayani hapa.

Mchungaji wa kanisa hilo, Jonas Msubi, alisema wametoa msaada huo ili kuonesha moyo wa upendo na kuwapunguzia changamoto za ukosefu wa mavazi watu hao.

Alisema msaada huo umetolewa na waumini hao kwa kuchanga kidogo kidogo ili waweze kutoa sadaka kwa wenzao wenye uhitaji waliopo katika kijiji hicho.

Alisema wataendeleza moyo huo wa kujitolea kusaidia jamii zenye mahitaji katika wilaya hiyo na maeneo mengine yenye watu wenye uhitaji kama hao.

Mariamu Joshua na Angelina Musa ni miongoni mwa watu wenye ukoma katika kituo hicho ambao walipata msaada huo, ambapo kwa nyakati tofauti walisema walikuwa na uhaba wa mavazi hivyo wanashukuru kanisa kwa kuguswa kuwasaidia.

“Tunawashukuru sana waumini wa kanisa hilo kwa moyo wao wa upendo, msaada huo utatusaidia sana kwani wengi wetu tulikuwa na uhaba wa mavazi,” alisema Angelina.

Alisema kwa sasa wana changamoto ya chakula hasa mahindi kwa kuwa mwaka huu mvua zimenyesha sana hivyo kuambulia mpunga tu hivyo waliomba jamii kuwasaidia mahindi ili kukidhi mahitaji yao ya chakula.

Awali akipokea msaada huo, Mchungaji Yusufu Sarangi wa misheni ya Iduguta, alilishukuru kanisa hilo kwa msaada huo wa nguo na kuongeza kuwa wasichoke kuwasaidia kwa kile watakachojaliwa ikiwemo chakula.

Kwa upande wa Mchungaji Msubi aliahidi kanisa lake litaangalia uwezekano wa kuwasaidia mahindi kama walivyoomba huku akisisitiza kuwa lengo lao ni kuendelea kudumisha umoja kati ya waumini wao na watu wenye mahitaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles