Mwandishi Wetu- Morogoro
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ametoa onyo kali kwa wakandarasi waliozembea kukamilisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro.
Kusaya alitoa onyo hilo jana, alipoongoza wajumbe wa kamati ya tendaji ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza thamani zao la mpunga katika mkoa huo.
Makatibu wakuu wengine walioshiriki ziara hiyo, ni Profesa Riziki Shemdoe (Viwanda na Biashara) pia Naibu Katibu Mkuu, Balozi Joseph Sokoine (Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Naibu Katibu Mkuu Gerald Mweli (Ofisi ya Rais-Tamisemi)
“ Hatujaridhishwa kabisa na wakandarasi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka ya Kijiji cha Mbogom Komtonga na Kigugu kwa kutokamilisha kazi ndani ya mkataba ” alisema kwa niaba ya kamati hiyo.
Katika hali isiyo ya kawaida kamati hiyo, ilichukizwa na kitendo cha mkandarasi M/s AMI & VAI Investment ya Dar es Salaam anayejenga ghala la kuhifadhia mpunga kijiji cha Kigugu wilayani Mvomelo kwa gharama ya Sh milioni 816.37, kukimbia eneo la mradi, licha ya kuwa na taarifa za ujio wa makatibu wakuu alikuwa nazo.
Alipoulizwa alipo mkandarasi wa mradi huo,msimamizi wa mafundi, Abdul Kabanika alisema “ Bosi tulikuwa naye hapa muda mfupi uliopita,sasa hatumuoni,”
Taarifa zilisema kampuni ya M/s Ami &Vai Investment, imeshindwa kumaliza kazi ndani ya mkataba ulioisha Aprili 21, mwaka huu na ujenzi upo asilimia 70 .
“Natoa muda hadi ifikiapo saa 11 jioni leo (jana) mkandarasi M/s AMI & VAI Investment awe amejisalimisha kwangu, ajue Serikali ina mkono mrefu.Tutamsaka kotote na kumrejesha hapa Kigugu atueleze kwanini kazi yetu hajakamilisha,” alisema Kusaya.
Kamati ilikagua pia mradi wa ghala kijiji cha Mbogo Komtongo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 70 chini ya mkandarasi M/s Shekemu kwa gharama ya Sh milioni 790.87, lakini haujakamilika.