30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Masoko ya madini yaongeza makusanyo kwa asilimi 200 Singida

Na Mwandishi wetu, Singida

AFISA Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Chone Malembo, amesema kuanzishwa kwa masoko ya madini katika mkoa huo, kumesaidia kupandisha makusanyo na kufikia Sh bilioni 3.243 ambayo ni sawa na asilimia 216.2 kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Malembo alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 ofisi yake ilipangiwa lengo la kukusanya Sh bilioni 1.5 lakini hadi Machi mwaka huu, walikuwa wamekusanya Sh bilioni 3.243 sawa na asilimia 216.2.

Alisema siri ya makusanyo hao ni pamoja na usimamizi mzuri kwenye masoko mawili ya madini yaliyoanzishwa Shelui Wilayani Iramba na Manispaa ya Singida mkoani Singida.

Akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kabla ya kuanzishwa kwa masoko husika Malembo alisema, katika mwaka wa fedha 2018/19, ofisi yake ilipangiwa lengo la kukusanya Sh bilioni moja lakini walikusanya Sh milioni 804.5.

Alisema mafanikio yaliyopatikana sasa ni mazao ya uwepo wa uwazi, uwajibikaji na ushirikiano  thabiti wa Serikali kwa ujumla wake na kwa msaada mkubwa wa viongozi wa wilaya na halmashauri zote.

Akizungumzia namna ofisi yake inavyodhibiti utoroshaji wa madini alisema kuwa mkoa umeanzisha Kikosi Kazi Madini (KKM) ambacho kina wajumbe kutoka taasisi muhimu ikiwemo baadhi ya taasisi zinazounda kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Alisisitiza kikosi kazi hukutana mara kwa mara ili kupitia taarifa na kujadili na kisha kutengeneza mikakati madhubuti inayosaidia udhibiti  wa utoroshaji wa madini na ukwepaji wa kulipa tozo za Serikali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel  Luhahula, akielezea mchango wa sekta ya madini katika wilaya yake, alisema mapato katika halmashauri ya Iramba yameongezeka hadi Sh milioni 99 tofauti na awali ambapo walikuwa wakipata Sh 500,000 kwa mwaka.

Alisema uanzishwaji wa masoko ya madini umepunguza kwa kiasi kikubwa cha utoroshaji wa madini kwa kuwa wachimbaji wa madini wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuyatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa  na kupata faida huku Serikali ikipata kodi mbalimbali.

Luhahula alitaja mafanikio mengine ya masoko ya madini yaliyoanzishwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha katika Wilaya ya Iramba  na kuwataka wachimbaji kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini huku wakijikinga na ugonjwa wa korona.

Akizungumza kwa niamba ya wachimbaji wa madini, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Kisonga na Shelui (UWAWAKISHE), Masumbuko Jumanne, alisema kuanzishwa kwa masoko ya madini kumeleta manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuuza madini yao kwa kufuata bei elekezi zinazotolewa na Serikali kila mwezi na kupata faida na  usalama kwenye biashara ya madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles