KESI ya kupinga matokeo ya ubunge wa Longido yaliyompa ushindi Onesmo Ole Nangole (Chadema), iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Stephen Kiruswa, imeanza kusikilizwa.
Nangole ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, ambaye alitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na upinzani, aligombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kufanikiwa kushinda.
Kesi hiyo iliyopo mbele ya Jaji Methew Mwaimu, jana  ilianza kusikilizwa kwa hoja zilizowasilishwa na upande wa Serikali.
Akiwasilisha hoja hizo, Wakili wa Serikali, Fortunatus Mhalila anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi, aliiomba mahakama kuondoa katika maombi ya mashtaka, kifungu cha 9(iv) ambacho ni fomu 21 B ya matokeo yaliyotangazwa akidai haina ubishani kwenye shauri hilo.
Katika hoja hizo, Wakili Mhalila aliweka pingamizi na kuomba upande wa mashtaka katika kesi hiyo kuondoa kifungu cha 9(ix) kinachosema magari ya Chadema na wafuasi wao yalitumika kukusanya masanduku ya kura.
Kutokana na hoja hizo, Jaji Mwaimu alipanga kutoa uamuzi wa shauri hilo la ama kuondoa au kutoondoa vifungu vilivyowasilishwa mahakamani hapo Januari 7, mwaka huu hatua itakayowezesha kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi.
Dk. Kiruswa anawakilishwa na Wakili Daud Haraka akisaidiana na mawakili Samson Lumende na Edmund Ngemela, ambapo mlalamakaji huyo anadai uchaguzi uliompa ushindi Nangole ulitawaliwa na dosari mbalimbali.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo mbali na Nangole, ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Longido.
Katika kesi hiyo, Nangole anawakilishwa na jopo la mawakili waandamizi ambao ni Method Kimomogoro, John Materu na Sheck Mfinanga.