Na DERICK MILTON-SIMIYU
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, ameagiza watu watakaobainika kuharibu miundombinu ya mawasiliano ya Shirika la Mawasiliano ( TTCL ) kuwafungulia kesi ya uhujumu.
Alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuboresha shirika hilo na miundombinu yake lakini kuna baadhi ya watu wanaihujumu ikiwemo kukata nyaya.
Alitoa agizo halo jana wakati akifungua jengo la TTCL la huduma kwa wateja Mkoa wa Simiyu, hafla iliyofanyika mjini Bariadi.
Alisema shirika hilo linakabiliwa na changamoto ya uharibifu na matumizi mabaya ya miundombinu ya mawasiliano, hivyo ili kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa, shirika na vyombo vya dola liwafungulie kesi za uhujumu uchumi watakaobainika kufanya uhalibifu huo.
“Wamesema hapa kuwa kuna changamoto ya kuharibiwa kwa miundombinu ikiwemo kukatwa nyaya na mambo mengine, sasa wewe unaletewa huduma kwenye eneo lako halafu unaenda kuharibu, huu ni uhujumu uchumi.
“Wale wataaobainika kuharibu miundombinu yenu washitakiwe kwa makosa ya uhujumu uchumi, wananchi hakikisheni mnakuwa walinzi wa miundombinu ya shirika,”alisema Samia.
Alilitaka shirika hilo kuongeza ufanisi wa huduma zeke kwani baadhi haziko vizuri, akitolea mfano huduma ya mtandao (internet) ambayo hata kwake imekuwa ikisumbua.
Aidha aliwataka wananchi wa Simiyu hasa wakulima wa pamba kuhakikisha wanatumia huduma za shirika hilo katika kupata taarifa za masoko na bei ya zao hilo.
Samia aliliagiza shirika hilo kuhakikisha wanapeleka mkongo wa mawasiliano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu ili kuboresha utoaji wa taarifa za wagonjwa .
Awali akitoa taarifa ya jengo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema awali shirika hilo lilikuwa likiongoza kwa kuwa na majengo mabovu lakini kwa sasa wamejitahidi kuwa na majengo ya kisasa.
“Shirika kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Simiyu walizindua mfumo wa kuwasaidia wakulima wa pamba kutunza pesa zao sehemu salama ambapo mpaka sasa umesajili wakulima zaidi ya 300,000 kutoka Amcos 383,”alisema Kindamba.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, alisema shirika limeendelea kuimarika hatua kwa hatua kwani limekuwa likitoa gawio kwa serikali kwa miaka miwili mfululizo.