MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amezindua mfumo wa TANESCO Mtandao (TANESCO App), mfumo ambao utaboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wateja pamoja na kudhibiti vishoka ndani ya shirika.
Akizindua mfumo huo, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Dk. Kalemani alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuiwezesha shirika kufanya kazi kwa ufanisi na sekta ya nishati kuwa injini katika Tanzania ya Viwanda.
Pamoja na hilo, pia aliipongeza bodi ya wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi kwa kufikia hatua ya kuanzia mfumo huo ambao utasaidia kuharakisha huduma kwa wateja.
Alisema mbali ya mfumo kulenga kuharakisha huduma kwa wateja, pia utapunguza gharama kwa wateja, kuongeza ufanisi kwa watumishi wake kuongeza mapato ya shirika.
Alizitaka taasisi zilizo chini ya wizara yake, kuutumia mfumo wa TANESCO App katika masuala mbalimbali.
“Ninajua sasa TANESCO hamlali,mnafanya kazi kubwa, makusanyo yameongezeka mara dufu kutoka Shilingi bilioni 11 kwa wiki kwa mwaka 2015/16 hadi bilioni 47, haya ni mafanikio makubwa. Ingawa nataka mfike kukusanya Shilingi bilioni 67 kwa wiki kwani hii pia itaongeza kutoka gawio zaidi kwa Serikali, “ alisema Dk. Kalemani
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dk. Alexander Kyaruzi alisema bodi imefarijika kwa ujio wa TANESCO App utaboresha uhusiano kati ya shirika na wteja.
Mkurugenzi Mtendaji shirika hilo, Dk. Tito Mwinuka alisema kuzinduliwa kwa App hiyo ni moja ya juhudi za Dk. Kalemani.
Alisema shirika kwa kutambua mchango wa wateja na changamoto mbalimbali ambazo wateja wamekuwa wakizipitia, uongozi uliona ipo haja ya kuanzisha mfumo ambao utawezesha kuwapatia huduma stahiki wateja katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.