27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kizimbani kwa kughushi mkataba ili kupata zabuni ya kujenga barabara

Kulwa Mzee

SERIKALI imewafikisha mahakamani wakurugenzi watatu wa Kampuni ya Civmark Ltd na wakili mmoja kwa tuhuma za kughushi mkataba kwa lengo la kupata zabuni ya kujenga barabara ya Manispaa ya Bukoba kwa kiwango cha lami.

Washtakiwa hao walifikishwa jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Rashid Chaungu.

Wakili wa Serikali, Adolf Lema aliwataja washtakiwa kuwa ni Crispin Mwombeki na Hadija Nyumbwe ambao ni mke na mume, Joseph Nyamwero na Wakili Glory Benne.

Wakili Lema alidai Septemba 17, 2017 maeneo ya Dar es Salaam, Mwombeki na Nyamwero kwa nia ya kudanganya, walighushi mkataba wa makubaliano ya pamoja kuonyesha kuwa kampuni mbili za Civmark Ltd na Mecco Ltd zimekubaliana kuunda mkataba huo kwa jina la Civmark Mecco Jv kwa lengo la kupata zabuni ya kujenga barabara ya Rubya-Kanyamabogo.

Alidai Septemba 20, 2017 maeneo ya Dar es Salaam, washtakiwa Mwombeki, Nyumbwe na Benne kwa nia ya kudanganya walighushi nguvu ya uwakilishi wa kisheria kuonyesha kampuni hizo zimekubaliana kutoa nguvu ya uwakilishi wa kisheria kwa Nyamwero kuwawakilisha kwenye zabuni hiyo.

Katika shtaka linguine, inadaiwa Oktoba 10, 2017 maeneo ya Bukoba mkoani Kagera, walighushi nyaraka  kuonyesha Kampuni ya Mecco imekubali kutoa nguvu ya uwakilishi wa kisheria kwa Nyamwero kuiwakilisha kampuni katika zabuni ya ujenzi wa barabara ya Manispaa ya Bukoba kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa tano.

Inadaiwa Mwombeki akiwa maeneo ya Bukoba alighushi nyaraka kuonesha kuwa kampuni ya Mecco Ltd ina uwezo wa kutengeneza barabara ya manispaa hiyo kwa kiwango cha lami.

Washtakiwa wote walikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana endapo watakidhi masharti.

Wakili wa utetezi, Paschal Kamala aliiomba mahakama hiyo iwape wateja wake masharti nafuu ya dhamana kwa sababu kwa miaka mitatu wamekuwa wakiripoti polisi bila kukosa.

Mahakama iliwataka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka Serikali za mitaa, nakala ya kitambulisho na kusaini ahadi ya Sh milioni tano.

Washtakiwa wote wameachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti na kesi iliahirishwa hadi Februari 26, kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles