Christina Gauluhanga , Dar es salaam
WAKATI watu waliofariki kutokana na virusi vya corona wakifikia 213 nchini china na wengine zaidi ya 10, wakithibitishwa kuwa virusi hivyo China na kwenye mataifa mengine, abiria wanaorejea nchini kutoka mataifa mbalimbali, wametakiwa kujitenga na familia zao kwa siku 14 ili kubaini kama wana virusi hivyo.
Tahadhali hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khalid Massa, wakati akitoa taarifa kwa wandishi wa Habari kuhusu kikao mkakati cha wadau wa mashirika ya ndege ya nchini na Kimataifa na wadau wengine kilichofanyika ambacho kililenga kudhibiti ugonjwa huo usisambae nchini.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, dalili za ugonjwa huo baada ya siku 14.
Alisema Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya ndege, wameimarisha ulinzi na kuweka vifaa muhimu vya kupima afya kwa abiria wanaoingia nchini na ambao wanazidi nyuzi joto 38 watawekwa kwenye kambi maalum ya uchunguzi.
“Tumejipanga kudhibiti ugonjwa huu kwakuwapima abiria wote wanaoingia nchini na ndege lakini pia kwakuwa dalili za ugonjwa huu zinaanza kuonekana baada ya siku 14, tunashauri wasafiri wanazotoka mataifa mbalimbali kujitenga na familia zao kwa siku 14 ili waweze kujichunguza afya,”alisema Dk Massa.
“Huenda wamepata maambukizo na dalili hazijaanza kuonekana kwa sababu zinaonekana baada ya siku 14 hivyo ili wawe salama na wasiambukize familia zao ni vema wakajitenga kwa muda huo,”alisema Massa.
Alisema pia endapo watabaini hali ya homa, joto, kukohoa au mafua wafike vituo vya afya vilivyopo jirani na na kuelezea historia ya safari zao ili wapatiwe matibabu.
Alisema wamedhamiria kutekeleza agizo la Serikali la kudhiti ugonjwa huo mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote nchini anayehisiwa kupata maambukizo hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Nchini, Hamza Johari, alisema Tanzania ni moja ya nchi inayotekeleza mikataba ya kimataifa ambayo pia inasisitiza kuzuia magonjwa ya kuambukiza.
Alisema tayari wameanza mikakati ya kuzuia ugonjwa huo na hatua za kuchukua ili kudhibiti maambukizo.
Alisema tathimini tayari ikifanyika ya viwango vya Anga na Shirika la Afya Duniani (WHO), hivyo hawana shaka kwakuwa kuna vipimo maalum na watumishi waliopewa mafunzo ya afya.