Mwandishi Wetu – Mjini Mgharibi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameungana pamoja na Vijana wa Halaiki na wahamasishaji walioshiriki katika maadhimisho ya sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika chakula maalum alichowaandalia.
Chakula hicho maalum cha mchana aliwaandalia kinatokana na ushiriki wao kwenye sherehe hizo za miaka 56, zilizofanyika January, 12 mwaka huu katika Uwanja wa Amani,mjini Unguja.
Hafla hiyo ilifanyika jana katika viwanja vya Polisi Ziwani na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma.
Wengine ni pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri, Naibu Mawaziri pamoja na Washauri wa Rais wa Zanzibar.
Katika shukrani zake Rais Dk. Shein kwa vijana hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi ‘Gavu’, alisema ana imani kubwa kuwa vijana hao watakuwa sehemu ya ulinzi wa Taifa hili kutokana na kujitowa kwao na uzalendo waliouonesha.
Alisema katika kipindi chote cha maandalizi ya sherehe hizo vijana hao walikuwa wakipokea vyema maelekezo wanayopewa na Viongozi wao na kuyafanyia kazi kwa maslahi ya taifa.
Aliwatakiwa kheri na mafanikio katika masomo yao ili waweze kufaidika katika maisha yao na kulisaidia Taifa kupiga hatua za kimaendeleo.
Aidha, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa uongozi wake madhubuti uliopelekea kuwepo kwa amani na utulivu, umoja na mshikamano, na kusema umesaidia sana kuharakisha maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.
Naye, Katibu wa Halaiki na Uhamasishaji, Ali Mohamed Baraka alitoa shukurani za dhati kwa Rias Dk. Shein kwa mwaliko huo na kutoa ahadi ya vijana hao kuendelea kushirikiana na Serikali ili kufanikisha vyema shughuli zinazoandaliwa.
Aidha, alimshukuru Rais Dk. Shein kwa kuwa karibu na vijana hao na kuonyesha imani upendo mkubwa kwao.