Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MRADI wa nyumba wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam, umekuja na suluhisho kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini.
Kutokana na hali hiyo tayari wanafunzi 4,317 wa vyuo sita vya elimu ya juu wataanza kuishi katika nyumba hizo za Mtoani Kijichi.
Hayo alisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyumba za mradi wa NSSF kwa ajili ya malazi kwa wanafuzi wa vyuo vya elimu ya juu, ambapo alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imejitahidi kuboresha mazingira ya elimu na taasisi zake.
Alisema uboreshaji huo umepelekea upanuzi wa udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu ongezeko hili limepelekea tatizo la uhaba wa malazi kwa wanafunzi.
“Mtakubaliana na mimi kuwa uboreshaji mazingira elimu na taasisi za elimu nchini kwahiyo uboreshaji wa elimu na taasisi zake umepelekea upanuzi wa udahili wa wanafunzi katika vyuo vyetu vya elimu ya juu lakini sasa ongezeko la udahili limeongeza tatizo la makazi ya wanafunzi,” alisema Mhagama
Alisema kuwa NSSF imeamua kuwa jibu sahihi na kwa wakati sahihi la kuondoa tatizo la malazi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini .
Mradi huo wa Mtoni Kijichi unatarajia kunufaisha wanafunzi 4,317 amabapo ni awamu ya kwanza. Katika awamu ya kwanza Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kitachukua wanafnzi 815,Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere majengo 1,398, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT) 144, Taasisi ya Uhasibu (TIA)1,165 Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) 699 na Chuo cha Diplomasia 96.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, alisema hii ni hatua nyingine ya Serikali ya Awamu ya Tano inavyoonesha dhamira yake ya dhati ya kuwajali wanyonge na kuboresha mazingira ya elimu.
Alisema asilimia 80 ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanakaa nje ya vyuo wanavyosoma na hivyo tatizo hili huwafanya wanafunzi kuishi kwenye nyumba za kupanga ambazo si rafiki na salama kwao.
“Tumeshuhudia matukio kadhaa ya wanafunzi kuvamiwa na vibaka na kuporwa vitu vyao na hata wakati mwingine huweza kuwaweka wanafunzi wa kike katika mazingira hatarishi,” alisema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio ameishukuru Serikali kwa muongozo uliowawezesha kufanikisha hatua ya ukamilishaji ya ujenzi kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huu kwa kuweka miundombinu ya maji safi na maji taka na umeme
Erio aliongeza kwa kuishukuru Serikali kwa muongozo wa kutumia “Force Account’ kwani utaratibu huu umewazesha kukamilisha mradi kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo cha Diplomasia, Xavery Andreas aliishuruku serikali kwa kutatua changamoto za wanafunzi.
Xavery amewataka wanafunzi wenzake washirikiane na NSSF kwa kuyatumia majengo hayo kwa usahihi.
NSSF inaendelea kulinda thamani ya michango pamoja na kuboresha mafao kwa wanachama wake kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo.