LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Tottenham, Jose Mourinho ameendelea kusotea ushindi baada ya jana kulazimishwa suluhu na Watford katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa kwenye Uwanja wa Vicarage Road, Watford.
Huo ni mchezo wanne mfululizo kwa Tottenham kushindwa kuvuna pointi pointi tatu, mara mwisho kushinda ilikuwa Disemba 26 mwaka jana, ilipoichapa Brighton mabao 2-1.
Baada ya mchezo huo, Tottenham ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Nowrich, ikachapwa bao 1-0 na Southampton, kabla ya kukubali kichapo kama hicho kutoka kwa Liverpool.
Kabla ya mchezo huo, Mourinho alitoka kuiongoza Tottenham kuvuna ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Middlesbrough katika mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la FA.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 31, baada ya kucheza michezo 23, pointi 30 nyuma ya Liverpool inayoongoza katika msimamo, ikiwa imecheza michezo 21.
Kikosi hicho kimekuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo baada ya kuumia kwa mshambuliaji wao, Harry Kane.
Hata hivyo, Watford watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia vema nafasi ya mkwaju wa penaltii, lakini nahodha wa kikosi hicho, Troy Deeney alipoteza penaltii hiyo iliyotokana na beki wa Tottenham, Jan Vertonghen kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Licha ya timu zote kufanya mabadiliko , ambapo Mourinho alimtoa Delle Alli na nafasi yake kuchukuliwa na Christian Eriksen,huku Gedson Fernandes akiingia kwa mara kwanza kuchukua nafasi ya Le Celso.
Watford nayo ilimtoa Ismailia Sarr na nafasi yake kuchukuliwa na Ignacio Pussetto.
Hadi dakika 90 za mtanange huo zinakamilika timu hizo zilitioka uwanjani zikigawana pointi moja kila mmoja baada ya kumaliza kwa sare ya 0-0.