Eymael, Sven watamaliza msimu salama?

0
753

Na WINFRIDA MTOI

SIMBA na Yanga ndizo klabu pekee zilizoliteka soka la Tanzania, ikichangiwa na idadi kubwa ya mashabiki wenye hisia kali na timu zao.

Mashabiki wa timu hizo ambao ni Watani wa jadi, hawafichi hisia zao sehemu yoyote pale kikosi chao kinapofanya vizuri au vibaya, lazima itafahamika wazi ni nini kimetokea.

Kitu  kinachozifanya timu hizi kuendelea kutawala soka la Tanzania ni kutokana na kuwa na wapenzi na wadau wa rika zote, wanaume kwa wanawake na hata viongozi wa taasisi mbalimbali binafsi na serikali.

Hali hiyo inazijengea timu hizi kuwa hazina kubwa ya watu ambayo wakati mwingine wanakuwa msaada mkubwa kwa klabu zao, lakini siku nyingine wakiamua kucharuka wanacharuka kwa pamoja.

Wadau na wapenzi wa Simba na Yanga kawaida yao wanapenda furaha, hasa kupata matokeo mazuri uwanjani, fikra zao wamezijengea kuwa timu zao si za kufungwa kirahisi.

Tabia hiyo ambayo imejengeka hata kwa viongozi wa klabu hizo, imewafanya makocha  wanaopewa majukumu  ya kuzinoa wawe katika wakati mgumu na wakidumu zaidi ya misimu miwili ni bahati.

Mara nyingi kocha wa timu hizo ataoneka mzuri na mwenye kiwango cha juu, pale  tu timu inaposhinda, lakini itokee siku moja ameboronga basi hugeuziwa kibao bila kujali nyuma alifanya mazuri kwa kiwango gani.

Mfano mzuri makocha waliofukuzwa msimu huu, Patrick Aussems na Mwingi Zahera, waliziteka akili za mashabiki wa timu hizo kutokana na mambo mazuri waliyowafanya.

Zahera alikuwa shujaa wa Yanga, baada ya kuhudumu Yanga iliyokuwa hoi taabu kiuchumi.

Katika msimu wake wa kwanza, Zahera aliiongoza Yanga kumaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Pia alifanikiwa kuwateka wapenzi wa timu hiyo kutokana na maneno yake ya kuwapa moyo pamoja na kujitoa huku akiwajengea ujasiri wachezaji wake wa kupambana katika mazingira magumu.

Alishiriki kuchanga fedha pale alipoona mambo yanakwenda vibaya.

Kwa upande wa Aussems alifanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kuitengenezea Simba rekodi ya pekee ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Hata hivyo,mwisho wa siku yote hayo yalionekana kwa uongozi wa  Simba ambao ulifikia uamuzi wa kumtimua.

Januari  2020 ilivyoanza

Mwaka huu klabu hizi mbili zimeuanza kwa kukutana katikamchezo wa kwanza wa Ligi Kuu, ziliposhuka dimbani kuumana Januari 4, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ilikuwa chini ya Charles Mkwasa aliyekuwa akikaimu nafasi ya Zahera, Simba  ilikuwa  na Mbelgiji Sven Vanderbroeck aliyerithi mikoba ya Aussems.

Mchezo huu ulikuwa wa maajabu kutokana na mambo yaliyotokea ndani ya dakika  90, ukiachana shabiki aliyeingia uwanjani wakati mechi inaendelea, gumzo kubwa lilikuwa matokeo ya sare ya 2-2 yaliyopatika.

Matokeo hayo yalikuwa ni shangwe kwa Wanayanga kwakua timu yao ilitanguliwa kufungwa kabla ya kusawazisha mabao yote mawili ndani ya dakika tatu.

Kitendo hicho kilikuwa mwiba mkali kwa Wanasimba, ambao tayari walikuwa wameamini wanachukua pointi tatu, hivyo uliibuka mjadala mkubwa kila mmoja akisema lake.

Kombe la Mapinduzi

Baada ya kuonyeshana ubabe katika mechi hiyo ya Ligi Kuu, kila mmoja alijipanga kwenda kulipa kisasi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kurudi na ubingwa.

Licha ya kupangwa makundi mawili tofauti, waliamini watakutana hatua yoyote kati ya nusu fainali au fainali, lakini bahati ikawa mbaya kwao.

Ilianza kutolewa Yanga katika michuano hiyo ilipokutana na Mtibwa Sugar na kufungwa kwa mikwaju 4-3 ya penalti.

Ikawa kicheko kwa Simba, lakini wakilaumu kwa nini mtani amewakimbia, bila kujua nao litawakuta kwani ilichapwa na Mtibwa na kushindwa kubeba kombe hilo.

Kitendo cha Simba kushindwa kuchukua kombe hilo, kulizua balaa kubwa baada ya   Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ kutangaza usiku huo huo kuachia ngazi.

Hata hivyo baadaye alibadili maamuzi hayo na kuendelea nafasi yake, lakini hali ilikuwa si shwari hata kwa mashabiki wakimlaumu kocha Sven kuwa hafai.

Zilivyorejea Ligi Kuu

Yanga imerejea Ligi Kuu ikianza na kocha mpya, Luc Eymael, mechi yake ya kwanza  tangu alipotua ardhi ya Tanzania alikutana na Kagera Sugar na kuanza kwa kichapo cha mabao 3-0.

Matokeo hayo yamewatibua Wanayanga, walianza kuhoji juu ya ubora wa kocha huyo, je ana uwezo wa kuwapa ubingwa kama wanavyotarajia?

Wanachojiuliza mashabiki, ni kwa nini kocha huyo amekubali kichapo cha mabao mengi hivyo ambayo hata Mkwasa aliyekuwa anasimamaia kwa muda katika mechi nane hajafungwa mabao kama hayo?

Mijadala hiyo inamuweka mashakani kocha huyo na kumfanya awe na kibarua kigumu cha kuhakikisha anawafurahisha Wanayanga kama walivyotarajia.

Pia kipigo hicho kiliwafanya mabosi wa Yanga kubadili uamuzi wa kumuacha straika wao David Molinga na kufanya jitihada za kurudisha jina lake katika usajili wa dirisha dogo dakika za mwisho.

Molinga alikuwa tayari yupo katika orodha ya wachezaji waliochwa dirisha dogo  na alishatangazwa lakini  siku aliibuka mazoezini.

Kwa upande wa kocha wa Simba, Sven, baada ya kushindwa katika michuano ya mapinduzi, ushindi wa mabao 2-1 alioupata dhidi ya Mbao, umeanza kurudisha imani za mashabiki kwake.

Mfululizo wa matukio katika timu hizi, yanatoa picha kuwa, hali bado haijatulia na inajulikana mara nyingi wanaotolewa kafara ni makocha, hivyo Wabelgiji hao wanatakiwa kujipanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here