25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaojisafisha kwa kuingiza vidole ukeni hatarini kupata saratani

AVELINE KITOMARY

SARATANI ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani inayotokea katika chembechembe za shingo ya kizazi, ambayo ni sehemu ya chini ya mji wa mimba (uteri) inayoungana na uke.

Aina mbalimbali za virusi aina ya papilloma wamethibitishwa kusababisha saratani hii ambayo hujitokeza kwa wingi miongoni mwa wanawake duniani kote, hususani wenye umri kati ya  miaka 20 hadi 39.

Saratani ya shingo ya kizazi ni ya pili miongoni mwa zile zinazowapata wanawake ambapo wagonjwa wapya wapatao 529,828 hugunduliwa kila mwaka sawa na asilimia 85 wakiwa ni katika nchi zinazoendelea.

Inabakia kuwa ya pili baada ya saratani ya matiti kwa kusababisha vifo vitokanavyo na saratani, ambapo huchangia asilimia 10 ya vifo vitokanavyo na saratani mbalimbali kwa wanawake. Inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake 275,000 hufa kila mwaka kwa ugonjwa huu, idadi kubwa ni kutoka nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.

AINA ZA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

Kuna aina mbili za seli kwenye shingo ya kizazi (cervix), ambazo ni squamous cell na glandular cells, hivyo saratani ambayo huanzia kwenye seli za squamous huitwa “squamous cell carcinoma” nainayoanzia kwenye seli za glandular huitwa “adenocarcinoma”. Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba inapoanza huwa ni vigumu kuigundua kwa sababu haioneshi dalili zozote, kwahiyo unaweza usigundue hadi pale inapofikia hatua mbaya, ambapo dalili kama kutokwa na majimaji au maumivu wakati wa tendo la ndoa huonekana.

Seli za saratani ya shingo ya kizazi  hukua taratibu na huchukua miaka michache kwa seli za kawaida kubadilika kuwa seli za saratani, ndio maana inashauriwa kufanya vipimo mara kwa mara ili kugundua mapema.

Akizungumzia ugonjwa huu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani wa Ocean Road, Dk. Julius Mwaisalage, anasema saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa kuwashambulia wanawake huku wengi wao wakichelewa kufika hospitalini kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dk. Mwaisalage, wagonjwa wengi hufika wakiwa na hatua ya tatu hadi ya nne, ambayo ni mbaya zaidi hii ni kutokana na sababu mbalimbali.

Januari ya kila mwaka, wataalamu wa magonjwa ya saratani huhamasisha upimaji na kutoa elimu kuhusu saratani ya mlango wa kizazi, ambapo huchochea wanawake kupima saratani.

Hata hivyo, kutokana na kampeni zinazoendelea kufanyika kuhamasisha upimaji wa saratani, wanawake wameonekana kuendelea kujitokeza kwa wingi.

MWAMKO WA KUPIMA

Wataalamu wanasema mwamko wa wanawake kupima saratani ya mlango wa kizazi sasa umeongezeka maradufu ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu kwa Umma, katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Maguha Stephano, anasema kwa kipindi cha mwaka jana, jumla ya wanawake 3,567 waliweza kupima saratani ya mlango wa kizazi ambapo kati yao 124 sawa na asilimia 7.3 walikutwa tayari wana mabadiliko ya awali ya saratani na 187 sawa na asilimia 5.2 walikutwa tayari wana ugonjwa huo.

Dk. Maguha anasema katika kipindi cha miaka ya nyuma, kutokana na mwamko mdogo wengi wao waligundulika wakati saratani ikiwa katika hatua za mwisho hali ambayo ilikuwa ngumu kupata matokeo mazuri ya tiba dhidi ya ugonjwa huo.

Ingawaje idadi ya wapimaji wa awali inaongezeka lakini bado kuna asilimia kubwa ya wanawake wanaochelewa hasa wale walioko maeneo ya mbali na huduma za afya au kutokuwapo kwa ugunduzi wa haraka wa saratani hiyo.

“Miaka ya nyuma ni wanawake wachache walikuwa wakija aidha wenyewe au kwa kuhamasishwa kuja kuchunguzwa afya zao, lakini leo hii kuna ongezeko kubwa.

Maguha ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani ORCI, anaongeza: “Hawa wenye mabadiliko ya awali tuliwapa tiba ili kuyazuia yasiwe saratani.

“Ambao tayari tuliwakuta na ugonjwa, tuliwaingiza kwenye mfumo wa matibabu, wanaendelea kutibiwa hapa ORCI,” anasema Dk. Maguha.

Anawashauri wanawake kuendelea kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara kujua mapema iwapo wamepata maambukizi, hii itawasaidi kuondokana na maumivu na vifo.

Anaishauri jamii kuhakikisha inawapeleka wasichana wadogo wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14 kupatiwa chanjo dhidi ya kirusi hicho katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Mwanamke hupata maambukizi ya kirusi hiki bila kujua. Kunasababu nyingi zinazofanya kirusi hiki kusababisha saratani, hivyo endapo wasichana watapata chanjo itakuwa rahisi kuepuka ugonjwa huo.

“Chanjo ya HPV ni salama, huchanjwa wasichana wadogo ili kuwakinga dhidi ya kirusi hiki, kwa sababu wengi huwa ni wale ambao bado hawajaanza kujihusisha na ngono hivyo hata watakapoanza itakuwa kinga kwao,” anasema.

WALIOKO HATARINI KUPATA

Dk. Maguha anasema kwa asilimia 99 saratani ya mlango wa kizazi husababishwa na kirusi cha HPV ambacho hutoka kwa mwanamume na kwenda kwa mwanamke kwa njia ya kujamiiana.

Anaeleza kuwa kwa kiasi kikubwa watu walioko hatarini zaidi ni mwanamume au mwanamke anayejihusisha na uhusiano wa mapenzi na zaidi ya mpenzi mmoja.

“Kihatarishi kingine ni msichana kuanza ngono katika umri mdogo, uvutaji wa sigara kwa wanawake, hii inaweza kufanya virusi hivyo kutengeneza saratani.

“Kuna sababu za kimaumbile au kijenetiki mfano kama mtu mwenye kinga ambayo iko chini, naye huwa hatarini kupata saratani.

“Watu wenye virusi vya Ukimwi nao wako hatari kupata saratani ya mlango wa kizazi kutokana na kushuka kwa kinga ya mwili, lakini hii haimaanishi kuwa kila mwenye kirusi hicho anapata saratani, bali hutegemea na kiwango chake cha kinga.

“Tafiti zinaonesha kuwa wale wanaojisafisha sehemu za uke kwa kujiingiza vidole wako hatarini kwa sababu huwa wanaondoa bakteria walinzi waliopo ukeni. Ukiwaondoa hao bakteria, virusi wanaweza kujibadilisha na kuwa saratani.

“Kuna wanawake wengine wanatabia ya kujiwekea vitu vyenye kemikali kama sabuni mara wengine wanaweka asali au ndimu ili kuwaridhisha wanaume, vitu hivi vinaua wale bakteria walioko sehemu za uke na vingine husababisha mchubuko, hivi vyote ni hatari kwa mwanamke,” anabainisha Dk. Maguha.

INATIBIKA

Kwa mujibu wa Dk. Maguha, endapo mgonjwa atawahi hospitalini mapema akiwa katika hatua ya kwanza na ya pili, anaweza kutibiwa na kupona kabisa aina hiyo ya satarani.

Anasema endapo mgonjwa atachelewa kufika hospitalini, uwezekano wa kupona kabisa huwa ni mdogo kutokana na kusambaa zaidi.

“Haya mabadiliko ya saratani huchukua muda mrefu kama miaka 15 hadi 20 kwa hatua ya kwanza. Hatua ya pili pia mgonjwa anaweza asione chochote, lakini ya tatu ya nne anaweza kuanza kuona dalili za kutokwa na damu wakati wa tendo la ndoa au kutokwa na damu isiyo ya hedhi.

“Ndio maana wanawake wanashauriwa kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi kila mwaka angalau mara mbili ili ukikutwa na saratani mapema uweze kutibiwa.

Hii ni kwa sasabu ukiwa hatua za mwanzo unapona kabisa, lakini ya tatu na nne huwezi kupona bali tutasaidia tu kupunguza maumiavu kwa dawa na mionzi,” anafafanua Dk. Maguha.

JUHUDI ZINAZOENDELEA

Kwa kipindi hiki kumekuwapo na ongezeko la wagonjwa wa saratani wanaofika hospitalini, hii ni kutokana na mwamko wa jamii kuelewa kuhusu vyanzo na athari za saratani kwa jamii na uchumi kwa ujumla.

Anasema katika kipindi cha miaka minne, wagonjwa waliopata huduma za uchunguzi na tiba waliongezeka kutoka 40,885 mwaka 2015/16 hadi kufikia 64,747 mwaka 2018/19.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani wa Ocean Road, Dk. Julius Mwaisalage, anasema licha ya wagonjwa wa saratani kuwa wengi, juhudi mbalimbali zinafanyika kuhakikisha wanapona.

Anasema sasa hivi kuna mafanikio makubwa katika sekta ya afya ambapo miundombinu imeboreshwa kama ujenzi wa vyumba maalum vya mashine za mionzi ‘bunkers’.

Anasema sasa hivi kuna mashine mbili za kisasa kwaajili ya tiba ya mionzi aina ya LINAC na CT stimulator.

“Mashine hizi zinatumia teknolojia ya 3D  na hupatikana katika hospitali yoyote kubwa ya saratani duniani,” anasema.

Anasema tangu mashine hizo kuanza kufanya kazi hapa nchini, jumla ya wagonjwa 1,141 wameshapatiwa matibabu ambapo wasingetibiwa takribani wagonjwa 208 wangepelekwa nje ya nchi.

“Gharama za kumtibu mgonjwa wa saratani nje ya nchi ni Sh milioni 50 hadi 75 ikuhusisha vipimo, tiba na kulazwa wodini.

“Mwaka 2015/16 wagonjwa 164 wa saratani walipatiwa rufaa kwenda nje ya nchi na mwaka 2017/2018 ni wagonjwa 25 walipatiwa rufaa, mwaka 217/18 na mwaka 2018/19 ni wagonjwa 14 tu,” anaeleza Dk. Mwaisalage.

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles