29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

TCRA, Nida waanika siri kukwama usajili laini

BENJAMIN MASESE-MWANZA

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) zimeeleza sababu zilizochangia wengi kushindwa kusajili laini za simu zao kwa wakati.

Zimesema hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana, laini za simu zilizokuwa zimesajiliwa  kwa njia ya alama za vidole (biometric) ni 24,021,757 kati ya 48,321,949 zinazotumika  nchini, ikiwa ni sawa na asilimia 49.7.

Pia taasisi hizo zimesema kitendo cha  Rais Dk. John Magufuli kuongeza siku 20  usajili wa laini za simu, kumeibuka wimbi la uhalifu na utapeli wa mamilioni ya fedha katika akaunti za benki na kupitia mawakala.

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja uliohusisha Nida, TCRA, Polisi na wawakilishi wa kampuni zote za mawasiliano Kanda ya Ziwa, walisema tatizo kubwa linalosababisha  Watanzania kutopata namba za vitambulisho vyao ni kutoa taarifa za uongo na kujisajili zaidi ya mara mbili kwa majina tofauti.

TCRA NA TAKWIMU

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, James Kilaba, Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo, alisema kama si agizo la Rais Magufuli kuongeza siku 20 za usajili, simu ambazo zilitakiwa kuwa hewani ni  24,021,757 kati ya 48,321,949 ya laini zote zinazotumika  nchini.

Mihayo alisema baada ya siku 20 zilizoongezwa, hawatakuwa na huruma tena kwa wale ambao wanatumia simu bila kukamilisha usajili kwa njia ya biometric, kwamba zitaondolewa kwenye mfumo wa mawasiliano.

“Nimewaita hapa kutoa taarifa juu ya usajili wa laini za simu kwa njia ya biometric, lakini nazungumza nanyi kwa niaba ya Mkurugenzi wa TCRA  mhandisi Kilaba, tumelazimika kufanya hivyo kwa sababu baada ya siku kuisha za usajili,  tumegundua waliosajiliwa hata hawafiki asilimia 50 ya watumiaji wote wa simu.

 “Bahati nzuri Rais Magufuli ameongeza siku 20 za usajili na leo (juzi) ni siku ya tatu, hivyo bado siku 17 tu tunaziondoa  katika mfumo, sasa msongomano uliopo sasa katika ofisi za Nida na maeneo mengine umesababisha kuibuka wizi, utapeli na kwa kuwa polisi wapo hapa watasema vizuri.

 “Uhalifu huu unahusisha mawakala wa watoa huduma za mawasiliano, ambao wanatembea mitaani wakiwa na vikoti vya kampuni husika na kujifanya wanasajili, lakini wanakwenda mbele zaidi na kuomba namba za siri za akaunti ya benki kwa madai kuwa usajili huo unakwenda sambamba na uhakiki wa taarifa za akaunti za benki,” alisema Mihayo.

NIDA

Kwa upande wake, Meneja wa Nida kwa Kanda ya Ziwa, Raphael Manase, alisema licha ya kuwapo msongamano mkubwa katika ofisi zao, lakini aliweka wazi kwamba hali hiyo inasababishwa na watu wenyewe kujiandikisha zaidi ya mara mbili kwa kutumia taarifa tofauti, hususan watumishi.

Manase alisema  watu wengi  wanaofika vituoni wanagundulika taarifa zao si za kweli na wanaondolewa katika mfumo na wengine wamejisajili majina tofauti, wakiwamo watumishi wa umma, wastaafu ambao wana lengo la kukwepa  madeni na vitu vingine.

Hata hivyo, Manase alikwenda mbali na kushauri Rais Magufuli asiongeze muda mwingine wa usajili wa laini kwa sababu matatizo yanayotokea watu kutopata namba na kitambulisho cha Nida yanasababishwa na wananchi wenyewe.

“Kwa kweli kuna watu ambao hawataki kujishughulisha kufuatilia namba za kitambulisho, kwani mfumo wa kuzipata umerahisishwa sana kupitia simu za mkononi, wapo wengine wanafika vituoni kufuatilia, lakini vitambulisho vyao vipo kwenye kata na anapofika ofisini tukiingia tunakuta tayari kitambulisho chake kipo.

“Wapo wengine wamefikia hatua ya kutushtaki ngazi za juu, eti sisi Nida tunasumbua au tunaomba rushwa, mfano pale ofisini wapo watu walijiandikisha zaidi ya mara nne kwa majina tofauti, kitambulisho chake kilishatoka na kipo kata, lakini anadai hajapata, tulipofuatilia tukabaini alishajiandikisha mara tatu kwa majina tofauti wakati kitambulisho kilishatoka.

“Katika hili kumeibuka utapeli na watu wametapeliwa sana, hadi matapeli wengine  wanajiita majina ya watumishi wa Nida na wanatoa namba halisi za watu, tumepigiwa (simu) na kudaiwa fedha au vitambulisho na tunapokutana na mwananchi mwenyewe wanakana mtu aliyekutana na kumtoza fedha si huyo mwenye namba aliyopewa,” alisema Manase.

Alisema Nida imeamua kufanya kazi siku zote zikiwamo za mapumziko na sikukuu ili waweze kuwahudumia wananchi ambao hawajapata namba au vitambulisho.

Aliwataka wananchi kutumia simu zao kupata namba kwa kuandika jina la kwanza, la mwisho, jina la mama la kwanza na la mwisho kisha kutuma kwenda namba 15069.

MAAGIZO YA SERIKALI

Juzi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni aliiagiza Nida kuongeza muda wa kufanya kazi ya uandikishaji na uchakataji wa taarifa kwa vitambulisho vya uraia kutoka saa nane hadi 16.

Alitoa agizo hilo kuhakikisha wananchi wanapata vitambulisho au namba kukamilisha usajili wa laini za simu zinazotarajiwa kufungwa baada ya Januari 20.

Pia aliwaagiza Nida kuhakikisha wanaongeza wafanyakazi (watendaji wa dharura) katika vituo vya kuandikishia ambavyo vipo katika kila wilaya nchini.

Masauni alitoa maagizo hayo alipotembelea ofisi za Nida Kibaha mkoani Pwani ili kujionea usajili unavyoendelea.

Pia alitangaza kufuta likizo na mapumziko ya mwisho wa juma kwa wafanyakazi wote wanaofanya kazi katika kitengo cha uchakataji wa taarifa za vitambulisho vya uraia ili kuwezesha wananchi wote kuvipata kwa wakati.

Alisema wameamua kuongeza muda wa ziada wa kufanya kazi kwa wafanyakazi hao baada ya kutembelea kitengo hicho na kubaini kuna changamoto ya wafanyakazi wachache na wanafanya kazi kwa saa chache, huku wananchi wakiendelea kuhangaika kupata vitambulisho ili kusajili laini zao.

“Lakini vitu ambavyo nimeviona vya msingi na tumekubaliana vifanyiwe kazi haraka, ni kitengo kinachohusika na uchakataji ama uchunguzi wa taarifa mbalimbali ambao kasi yao ni ndogo sana.

“Na  kasi hii ndogo inatokana na kwanza uchache wa wafanyakazi na pia uchache wa muda wa kufanya kazi, kwa maelekezo yangu na ambavyo tumekubaliana, kwanza wataongeza muda wa kufanya kazi kutoka saa nane hadi 16 kwa siku zote 18 na hakutakuwa na ‘holiday’ (likizo) wala hakutakuwa na ‘weekend’ (mapumziko ya siku za mwisho wa wiki),” alisema Masauni.

MATUKIO YA UTAPELI

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, limesema matukio ya utapeli unaohusisha usajili wa laini za simu yameongezeka maradufu baada ya Rais Magufuli kuongeza siku 20 za usajili huku mamilioni ya fedha yakichukuliwa benki baada ya kundi la vijana linalovalia vikoti vya kampuni za mawasiliano kutembelea watu majumbani na katika biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Nyamagana (Jiji), Juma Jumanne alisema takwimu zinaonyesha kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka jana matukio ya utapeli kuhusu usajili wa simu yalikuwa saba tu, lakini ghafla Desemba yalipanda.

 “Kwa mwezi Desemba wakati tunaelekea mwisho mwisho wa mwaka, kumeibuka matukio mengi ya utapeli unaohusisha usajili wa simu ambapo tumepokea matukio 23 ya kuibiwa fedha na simu zinazotumika kufanya miamala ya fedha, wanaofanya matukio hayo wanadaiwa kuwa ni vijana waliovalia vikoti vya makampuni ya mawasiliano.

“Baada ya Rais Magufuli kuongeza siku 20, unaweza kushangaa kwa Januari hii ya mwaka 2020, tumepokea matukio 30 ya wizi wa fedha yanayofanywa na kundi hilo hilo.

“Yupo mkazi aliyetapeliwa na kutoa namba ya siri ya benki na kuibiwa Sh milioni nne, mwingine Sh 900,000 na Sh milioni mbili na wengine.

 “Baadhi ya vijana hao tumewakamata, tena ni wadogo ambao wanajua kuchezea simu na wanazijua kweli.

“Pia tumepokea matukio ya mawakala ambao wanafanya miamala, ambao nao wameibiwa simu wanazofanyia miamala ya fedha ambazo zimeibwa, yaani kuna mteja anaiba simu kituo fulani, anatoa fedha zote kisha anakwenda anaiacha kituo kingine na kuchukua nyingine yenye fedha, sasa mwisho wa siku waliobiwa wanakutana polisi.

“Tunapofuatilia tunagundua mtu mmoja kaiba simu vituo viwili na simu ya kituo cha awali inapatikana kituo cha pili, hapo unaweza kuona mchezo uliopo ambapo mawakala wanaweza kudaiana wakati wote wameibiwa,” alisema Jumanne.

Alitoa wito kwa mawakala kuwa makini na wateja wanaokwenda kufanya miamala ya mara kwa mara kwani baadhi yao huangalia mazingira ya kuiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles