23 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Mechi za nyumbani zisiishie kwa Diamond, Harmonize

BEATRICE KAIZA

BABA na mwana yaani Diamond Platnumz na Harmonize, wamefanikiwa kuchota mapenzi makubwa kutoka kwa maelfu ya raia wanaoishi kwenye maeneo  wanayotokea wasanii hao.

Diamond Platnumz ambaye jana alirejea jijini Dar es Salaam  akitokea Kigoma kwa njia ya treni, alifunga mwaka akiwa Uwanja wa nyumbani, dimba la Lake Tanganyika akiongoza  jopo la wasanii nyota waliomshindikiza katika tamasha lake la kutumiza miaka 10 kwenye muziki.

Mafanikio makubwa ya tamasha hilo yalianza kuonekana mapema hata kabla Diamond hajafika mkoani Kigoma. Katikati ya safari, Diamond alilazimika kusimama na kuwasalimia mamia ya raia walikuwa wamekaa wakimsubiri kwa hamu.

Hata alipofika katika kituo kikuu cha treni Kigoma na kuvishwa mavazi ya kimila kisha kundi la popo wengi kuruka angani  ambapo wenyeji wakasema ni ishara kuwa mfalme ameingia. Mondi hakuwaacha hivi hivi mashabiki waliokuwa wamekusanyika stesheni hapo, ilimbidi apige shoo ya bure na umati wote wa  watu ulikuwa unaimba naye mwanzo mwisho jambo ambalo lilipongezwa na  mastaa wengi akiwamo Ne-Yo, mwimbaji wa Marekani.

Akiwa nyumbani kwao, Diamond alishiriki katika uzinduzi wa msikiti alioujenga pamoja na kufanya mambo mengi ya kijamii kwaajili ya wakazi wa mkoa wa Kigoma. Kwa kazi kubwa aliyoifanya Diamond alipata bahati ya kuufungua mwaka 2020 kwa kupigiwa simu na Rais Dk. John Magufuli aliyempongeza na kuwaahidi wananchi kuwa atawajengea kilomita 310 za barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kigoma kwenda Nyakanazi.

Ukiacha mafanikio ya tamasha la Diamond huko Kigoma, pande wa Mtwara anga lilikuwa limetawaliwa na Konde Boy aliyetua kuwapa mkono wa heri ya mwaka mpya ndugu zake ndani ya Uwanja wa Majaliwa, Tandahimba.

Ishu ilianza mapema kabisa  ambapo Harmonize aliingia nyumbani kwao Mtwara kwa usafiri wa helkopta na akatua katika viwanja vya shule ya msingi Matogoro. Aliposhuka maelfu ya wakazi wa mji huo walikusanyika kumpokea wakiongozwa na wazee wa kimila waliomfanya taratibu za jadi kwa kuchinja mbuzi na kumpaka damu, kisha akaondoka kuelekea kufanya maandalizi ya onyesho lake.

Usiku wa kuamkia mwaka mpya, Harmonize alifanikiwa kuiteka Tanzania kwani tamasha lake la Harmo Night lililokuwa linaruka ‘live’ kwenye moja ya kituo kikubwa cha runinga nchini. Kwanza Uwanja wa Majaliwa ulijaa nyomi, watu walilipa viingilio vyao kuanzia 10,000 mpaka 20,000 na Harmonize akaibuka na ubunifu wa aina yake kwa kuingia jukwaani akining’inia katika katikati ya mashabiki na kuwaimbisha nyimbo za kimakonde na ngoma yake Never Give Up.

WASANII WENGINE VIPI?

Katika hali ya utafutaji wasanii wengi maarufu unaowasikia hapa Tanzania, asili yao siyo Dar es Salaam. Walitoka mikoa tofauti tofauti kuja kutafuta maisha ila walipofanikiwa wakahamishia makazi yao DSM.

Kwa hizi shoo mbili kubwa za baba na mwana (Diamond na Harmonize), tunapata somo kuwa kuna utajiri mkubwa wa watu katika maeneo yetu ya asili hivyo wasanii wengine  si vibaya kuwaiga wawili hao ambao kiukweli wameichangamsha tasnia ya burudani kwa kuwa gumzo la kufungulia mwaka 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles