Na DEEICK MILTON-SIMIYU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Simiyu, imewatoa hofu askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, ambao wamekuwa na wasiwasi juu ya utekelezaji wa mfumo mpya wa kielektroniki unaofahamika kama ‘Takukuru App’ ambao utatumika kudhibiti vitendo vya rushwa.
Mfumo huo ambao ulizinduliwa Novemba, 2019 umelenga kuwadhibiti askari hao ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa ikiwa pamoja na kupunguza ajali za barabarani ambazo usababishwa na rushwa.
Wakizungumza wakati wa kikao na maofisa wa Takukuru kilichokuwa na lengo la kutambulisha mfumo huo, askari hao walionyesha wasiwasi wao juu ya ukweli na usahihi wa picha za video au mnato zitakazopigwa na wananchi kisha kutumwa Takukuru.
Askari hao walisema kuwa baadhi ya picha zinaweza kuwa za kweli lakini ni katika utoaji wa huduma kwa kufuata taratibu zilizopo na siyo rushwa, huku wakitaka kujua Takukuru walivyojipanga kuchambua ukweli na uongo.
“Kuna baadhi ya makosa au vitu vingine lazima mwenye gari alipie pesa, mfano stika, wakati huo askari unapokea malipo hayo na ukapigwa picha wakati jambo lenyewe ni halali kisha picha ikatumwa kwenu, je kuna nafasi ya uchunguzi au askari atapoteza kazi moja kwa moja maana itatafsiliwa kuwa ni Rishwa?,” alihoji PC Sufian Killo
Naye askari John Mrema alihofia mfumo huo kuwa na upendeleo kwa mtu mmoja ambaye ni askari mpokeaji na siyo kwa mtoaji, ikiwa pamoja na jambo lenyewe litakuwa ni kwa nia hovu ya kutaka kumwaribia kazi askari.
“Kama tunavyojua mfumo wa utumishi wa jeshi ni tofauti na sehemu nyingine, sijui Takukuru mmejipanga vipi kutusaidia ili picha ambazo zitatumwa zinafanyiwa uchunguzi kwanza, kwani ikionekana askari anapokea ela moja kwa moja watasema ni rushwa na atafukuzwa kazi kumbe ulikuwa mtego,” alihoji Mrema.
Akijibu hofu za askari hao Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Simiyu, Joshua Msuya alisema kuwa taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha kila picha inayowasilishwa kwao kupitia mfumo huo unafanyiwa uchunguzi kwanza kabla ya hatua kuchukuliwa.
“Ukiangalia kwenye mfumo wenyewe, mhusika wa kutuma picha anatakiwa kujisajili, mkoa gani anatoka, yupo wapi, majina yake, hayo yote ni katika kuhakikisha haki ipatikana kwa kila mtu,” alisema
Msuya alisema hakuna mtu ambaye atanyanyaswa na mfumo huo na wala haumlengi mtu, bali ni katika kupambana na vitendo vya rushwa kwa mtoaji na mpokeaji.
Mfumo huo wa ‘Takukuru App’ utawezesha wananchi kutuma taarifa za vitendo vya rushwa vinavyofanyika sehemu mbalimbali nchini kwenda Takukuru moja kwa moja ambapo utaanza kutumika rasmi Januari 2020.