Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA
WADAU wa elimu nchini wamehoji sababu mtaala wa elimu wa mwaka 2016, haukuwashirikisha walimu kabla ya Serikali kuupeleka shuleni.
Wakichangia mada iliyohusu mtazamo wa walimu kwa Mtaala wa elimu wa mwaka 2016, wadau hao walidai umekuwa na sintofahamunyingi huku wakitaka kujua ni kwanini haukuwashirikisha walimu kabla ya Serikali kuupeleka mashuleni.
Wadau hao walikuwa wakizungumza katika mkutano wa siku tatu ulioandaliwa na Mtandao wa Ten/Met.
Akiwasilisha mada hiyo, Mshauri wa Elimu kutoka Haki Elimu, Wildaforce Maina, alisema katika utafiti alioufanya mwaka 2018 amegundua walimu wengi hawana uelewa kuhusiana na mtaala wa elimu wa mwaka 2016.
“Nilifanya utafiti wangu mwaka 2018 na nilichogundua ni kwamba walimu wengi hawana uelewa kuhusiana na mtaala wa mwaka 2016, wengi wameukuta wakati wa kufundisha tu hawajui ukoje hivyo wamekuwa wakifundisha tu bora liende,”alisema.
Mshauri huyo wa elimu aliishauri Serikali kuwashirikisha walimu kunapokuwa na mabadiliko ya mitaala ili iwe rahisi kujua changamoto zipi ambazo zipo kwa walimu na wanafunzi.
Kwa upande wake, Meneja Programu kutoka Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAPIE), Laurent Gama, alisema mtaala wa elimu wa mwaka 2016 ulitangulia darasani kabla ya walimu hawajaujua unataka nini.
“Rai yangu mabadiliko lazima yaendane na mahitaji, lazima kuwe na vifaa vya utekelezaji, vifaa visichelewe kama ambayo mtaala unataka, lazima kuwe na usimamizi mzuri, lazima kuwe na vitabu, lakini ni lazima walimu wapate mafunzo,”alisema.
Naye, Mtaalamu wa elimu kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Peter Mlimahadala, alisema walimu kutoijua mitaala mapema, kunaathari kwa taifa.
“Walimu wao ndio wanaweza kueleza changamoto kwa sababu ndio wanaofundisha wao ndio wanatakiwa kutoa ushauri tunatakiwa tufundishaje, hili ni muhimu sana kwa taifa letu baadae tutakuwa na wataalamu ambao ni jina tu,”alisema.
Mwisho
Safari za treni Dar –Mosi zaongezwa
Na TUNU NASSOR
-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limeongeza safari mbili kwenye ratiba zake za njia mpya ya kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi.
Disemba 6, mwaka huu TRC walirudisha safari za abiria Dar es Salaam – Moshi ambazo zilikuwa zimesimama kwa miaka 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dra es Salaam jana, Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa, alisema wameamua kuongeza safari hizo baada ya kuwapo kwa maombi mengi kutoka kwa wadau.
“Kuanzia Jumatatu Disemba 16, ratiba ya safari za kutoka Dar kwenda Moshi itakuwa Jumatatu jumatano na Ijumaa,” alisema Kadogosa.
Alisema kwa safari za kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam zitakuwa Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.
Aliongeza kuwa kusafiri na usafiri wa treni utasaidia kupunguza ajali zinazotokea katika kipindi cha sikukuu kutokana na baadhi ya madereva kunywa pombe na kuendesha magari.
“Kwa kutumia usafiri huu utapunguza uvunjifu wa sheria za usalama barabarani na kupunguza ajali kutokana na wengi kusafiri kwa treni,” alisema Kadogosa.
Akizungumzia mafanikio ya shirika hilo, Kadogosa alisema TRC imefanikiwa kuongeza mapato kutoka Sh. Bilioni 17.4 mwka 2014/15 hadi kufikia Sh. bilioni 30.041 mwaka 2018/19 kwa treni za mizigo.
Alisema kwa treni za abiria wamefanikiwa kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 8.39 hadi kufikia Sh bilioni 10.774.
“Kwa abiria wa mijini imeongeza mapato kutoka Sh milioni 316.668 hadi kufikia Sh bilioni 1.968.
“Jumla tumefanikiwa kuongeza abiria kutoka 845,607 kwa mwaka 2014/15 hadi kufikia abiria 4,280,043 kwa mwaka 2018/19 kwa treni za mjini,” alisema Kadogosa.
Aliongeza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa Dar es Salaam kwenda Morogoro umefikia asilimia 70 na Morogoro kwenda Makutupora umefikia asilimia 20.
Alisema TRC imeweza kusafirisha tani 1,456,537 katika reli ya kati na abiria wa treni za mikoani wameongezeka kutoka 411,172 mwaka 2014/15 hadi kufikia abiria 578,439 kwa mwaka 2018/19.