NA THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
PAMOJA na ushindi wa mabao 3-2 ilioupata timu yake kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amesema kikosi kilikosa mawasiliano mazuri kati ya golikipa na mabeki.
Yanga iliibuka na ushindi huo, katika mchezo uliochezwa juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwenye mchezo huo, Mkwasa alimpanga Farouk Shikalo katika eneo la kipa, wakati mabeki walikuwa Japhary Mohamed aliyecheka upande wa kushoto na Juma Abdul kulia,huku Alli Sonso na Lamine Moro wakicheza kati.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkwasa alisema mawasiliano hafifu kati ya Shikalo na mabeki wake ndio chanzo cha kuruhusu mabao mawili ya JKT Tanzania.
“Tumepata ushindi muhimu wa pointi tatu kama ambavyo mpango wetu toka awali ulikuwa.
“Hata hivyo kulikuwa na matatizo ya mawasiliano kati ya golikipa na mabeki na kusababisha kuruhusu mabao ambayo kama wangejipanga vema tusingefungwa,”alisema.
Mkwasa ambaye anakaimu nafasi hiyo baada ya aliyekuwa anaishikilia Mwinyi Zahera kufungashiwa virago kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alikisifu kikosi chake akisema kinaendelea kuimarika siku baada ya siku.
Wakati huo huo, Mkwasa aliwasifu wapinzani wao kwenye mchezo wa juzi JKT Tanzania kwa kuonyesha kandanda zuri.
“Nililazimika kutumia viungo kadhaa kwakua wapinzani wetu walikuwa vizuri, mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa,”alisema Mkwasa.